Ingawa jambo la uponyaji wa Mungu lina utata kiasi fulani, si kitu kilichofichika katika Maandiko. Ukweli ni kwamba, kiasi cha moja ya kumi yakila kitu kilichoandikwa katika zile Injili nne kinahusu huduma ya uponyaji ya Yesu. Zipo ahadi za uponyaji wa Mungu katika Agano la Kale, Injili na katika nyaraka za Agano Jipya. Wale walio wagonjwa wanaweza kupokea faraja kubwa sana katika wingi wa maandiko yenye kujenga imani.
Nimeona katika safari zangu duniani kote kwamba, kwa ujumla, uponyaji wa Mungu ni kitu cha kawaida katika makanisa yaliyojaa waamini waliojitolea kikamilifu (wanafunzi wa kweli). Mahali ambapo kanisa limepoa na ni la kimaendeleo, uponyaji unatokea kwa nadra sana.[1] Hayo yote yasitushangaze kwa sababu Yesu alisema kwamba ishara moja itakayofuatana na waaminio ni kwamba wataweka mikono juu ya wagonjwa nao watapona (ona Marko 16:18). Tungepima makanisa kwa ishara ambazo Yesu alisema zitafuatana na waamini, tungefikia mahali pa kuamua kwamba makanisa mengi hayana waamini.
[Yesu] Akawaambia, Enendeni ulimwengu mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya (Marko 16:15-18).
Mtumishi afanyaye watu kuwa wanafunzi, akiwa anaiga huduma kamilifu ya Kristo, hakika atatumia vipawa vyake kuendeleza huduma ya uponyaji wa Mungu katika eneo lake la ushawishi. Anajua kwamba uponyaji wa Mungu hukuza ufalme wa Mungu kwa njia mbili. Kwanza – miujiza ya uponyaji ni matangazo mazuri sana kwa Injili, kama mtoto yeyote anayesoma Injili au kitabu cha Matendo atakavyoelewa (ingawa watumishi wengi wenye madigirii makubwa wanaonekana hawaelewi). Pili – wanafunzi wenye afya njema hawazuiwi kufanya huduma kwa magonjwa binafsi.
Pia, mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anahitaji kuwa makini kwa wale katika mwili wa Kristo wanaohitaji uponyaji, ila wana shida ya kupokea. Mara nyingi wanahitaji mafundisho ya taratibu na kutiwa moyo kwa upole, hasa kama wamefikia mahali pa kupingana na ujumbe wowote wa uponyaji. Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anakabiliwa na uchaguzi: anaweza kuepuka kufundisha kuhusu uponyaji wa Mungu moja kwa moja. Akifanya hivyo, hakuna atakayekwazika wala hakuna atakayeponywa. Au, anaweza, kwa upendo sana, kufundisha somo hilo na kudiriki kuwakwaza wengine huku akiwsaidia wengine kupokea uponyaji. Mimi binafsi nimeamua kufanya la pili, nikiamini kwamba ni kufuata mfano wa Yesu.
Uponyaji Pale Msalabani
Mahali pazuri pa kuanza kujifunza kuhusu uponyaji wa Mungu ni katika sura ya hamsini na tatu ya kitabu cha Isaya, ambayo huhesabika kuwa unabii kuhusu Masiya. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Isaya anaeleza vizuri sana juu ya kifo cha Yesu cha kujitoa dhabihu na kazi ambayo angetimiza msalabani.
Hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu. Lakini tuimdhania ya kuwa amepigwa, amepigwa na Mungu na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu. Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe, na BWANA ameweka juu yake maovu yetu sisi sote (Isaya 53:4-6).
Kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, Isaya alitangaza kwamba Yesu alibeba huzuni na masikitiko yetu. Tafsiri nzuri ya lugha ya asili ya Kiebrania inaonyesha kwamba Yesu alichukua magonjwa na maumivu yetu.
Neno la Kiebrania huzuni katika Isaya 53:4 ni neno choli, ambalo pia linapatikana katika Kumbu. 7:15; 28:61; 1Wafalme 17:17; 2Wafalme 1:2; 8:8; na 2Nyakati 16:12; 21:15. Katika maandiko haya yote linatafsiriwa kama magonjwa au maradhi.
Neno masikitiko katika Kiebrania ni makob, ambalo pia linapatikana katika Ayubu 14:22 na 33:19. Pote hapo linatafsiriwa maumivu.
Kwa hali hiyo, Isaya 53:4 inatafsiriwa vizuri kama ifuatavyo: “Hakika magonjwa yetu Yeye Mwenyewe aliyabeba, na maumivu yetu aliyachukua.” Ukweli huu unatiwa muhuri na Mathayo kurejea maneno ya Isaya 53:4 katika Injli yake, hivi: “Yeye Mwenyewe alichukua udhaifu wetu na kuyabeba maradhi yetu” (Mathayo 8:17, TLR).
Kwa kuwa si rahisi kuepuka kweli hizi, kuna wanaojaribu kutufanya tuamini kwamba Isaya alikuwa anasema juu ya “magonjwa ya kiroho” na “maradhi ya kiroho” tuliyo nayo. Lakini maneno ya Isaya 53:4 yanayotumiwa na Mathayo yanaonyesha bila shaka yoyote kwamba Isaya alikuwa anazungumzia magonjwa halisi ya kimwili na maradhi. Hebu tuyatazame katika mantiki yake.
Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, ‘Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na kuyachukua magonjwa yetu’ (Mathayo 8:16-17. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Mathayo alieleza waziwazikwamba uponyaji wa kimwili uliotendwa na Yesu ulikuwa kutimizwa kwa Isaya 53:4. Basi hakuna shaka kwamba Isaya 53:4 ni maandiko yanayosema kuhusu Kristo kuchukua udhaifu wetu na magonjwa.[2] Sawa na jinsi Maandiko yanavyosema kwamba Yesu alichukua maovu yetu (ona Isaya 53:11), yanasema pia kwamba alichukua maradhi yetu na udhaifu wetu. Hizo ni habari za kumfanya mgonjwa yeyote kufurahi. Kwa dhabihu Yake ya kupatanisha, Yesu alikwisha weka mpango kwa ajili ya sisi kupata wokovu na uponyaji.
Swali
Wengine wanauliza hivi: Kama hayo ni kweli, mbona si kila mtu anayeponywa? Jibu zuri ni kuuliza swali lingine: Mbona si watuwote waliozaliwa mara ya pili? Si wote waliozaliwa mara ya pili kw sababu, aidha hawajasikia Injili, au pengine hawajaiamini. Vivyo hivyo, kila mtu binafsi lazima ajipatie uponyaji wake kupitia imani yake. Wengi bado hawajasikia kweli hiyo ya kupendeza kwamba Yesu alichukua magonjwa yao. Wengine wamesikia lakini wamekataa.
Jinsi Mungu Baba anavyotazama magonjwa ni kitu kimedhihirishwa wazi kwa huduma ya Mwana Wake mpendwa, aliyejishuhudia mwenyewe kama ifuatavyo:
Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile (Yohana 5:19).
Tunasoma katika kitabu cha Waebrania kwamba Yesu alikuwa “mfano halisi wa asili Yake [Baba]” (Waebrania 1:3, TLR). Hakuna shaka kwamba jinsi Yesu alivyotazma magonjwa ni sawa na jinsi Baba Yake alivyotazama.
Yesua lionaje magonjwa? Hakuna hata mara moja ambapo alimrudisha yeyote aliyemjia akitaka kuponywa. Hakuna hata mara moja alipomwambia mtu aliyetaka kuponywa, “Si mapenzi ya Mungu wee uponywe, hivyo itabidi ubakie mgonjwa.” Kila wakati Yesu aliwaponya wagonjwa waliomjia, na mara walipoponywa, mara nyingi aliwaambia kwamba ni imani yao ndiyo imewaponya. Zaidi ya hayo, Biblia inatangaza kwamba Mungu habadiliki (ona Malaki 3:6) na kwamba Yesu Kristo ni “yule yule, jana, na leo na hata milele” (Waebrania 13:8).
Uponyaji Unatangazwa
Kwa bahati mbaya, wokovu siku hizi umechujwa na kubaki kuwa msamaha wa dhambi tu. Lakini maneno ya Kiyunani yanayosema kuhusu “kuokoka” na “wokovu” yana maana kubwa – si msamaha tu bali ukomozi kamili na uponyaji.[3] Hebu tumtazame mtu katika Biblia aliyepokea wokovu kwa ukamilifu. Yeye aliponywa na imani yake alipokuwa anamsikiliza Paulo akihubniri Injili mjini kwao.
Wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia, na nchi zilizo kando kando; wakakaa huko, wakiihubiri Injili. Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa. Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda (Matendo 14:6-10).
Ona kwamba ingawa Paulo alikuwa anahubiri “Injili”, yule mtu alisikia kitu kilichosababisha imani moyoni make ili apokee uponyaji wa mwili wake. Kwa kiasi kidogo, bila shaka alimsikia Paulo akisema kitu juu ya huduma ya Yesu ya uponyaji, na jinsi Yesu alivyomponya kila mtu aliyeomba uponyaji kwa imani. Pengine Paulo alitaja pia unabii wa Isaya kuhusu Yesu kuchukua magonjwa yetu na maradhi. Hatujui – lakini kwa kuwa “imani huja kwa kusikia” (Warumi 10:17), yule mtu aliyepooza pengine alisikia kitu kilichowasha moto imani katika moyo wake, kwamba ataponywa. Kitu fulani alichosema Paulo kilimshawishi kwamba Mungu hakutaka aendelee kupooza.
Bila shaka Paulo mwenyewe aliamini kwamba Mungu alitaka mtu huyo aponywe, la sivyo maneno yake yasingemshawishi mtu huyo kuwa na imai ya kuponywa, wala asingemwambia asimame. Je, kungeotkea nini kama Paulo angesema yale ambayo wahubiri wengi wa siku hizi wanasema? Ingekuwaje kama angehubiri hivi: “Si mapenzi ya Mungu kwa kila mtu kuponya”? Huyo mtu asingekuwa na imani ya kuponywa. Pengine hii inaeleza kwa nini watu wengi hawaponywi siku hizi. Wahubiri wale wale wanaotakiwa kuwahamasisha watu wawe na imani ya kuponywa, ndiyo wenye kuharibu imani hiyo.
Hapa tena ona kwamba mtu huyu aliponywa kwa imani yake. Kama asingeamini angebaki amepooza tu, hata ingawa ulikuwa ni mpango wa Mungu kwake kuponywa. Tena, pengine walikuwepo wagonjwa wengine pia katika kundi lile siku hiyo, lakini hatuambiwi yeyote mwingine kuponywa. Kama ni hivyo, mbona hawakuponywa? Kwa sababu ile ile iliyowazuia wengi wasio-okoka waliokuwepo katika kundi hilo kuokoka – kwa sababu hawakuamini ujumbe wa Paulo.
Hatupaswi kuamua kwamba si mapenzi ya Mungu kumponya kila mtu kwa kuwa kuna watu hawaponywi. Hiyo ni sawa na kuamua kwamba si mpaenzi ya Mungu kwa wote kuokoka kwa sababu watu wengine hawaokoki. Kila mtu lazima aiamini Injili kibinafsi kama anataka kuokoka, na kila mtu lazima aamini mwenywe kama anataka kuponywa.
Uthibitisho Zaidi Kwamba Ni Mapenzi Ya Mungu Kuponya
Chini ya agano la zamani, uponyaji wa mwili ulikuwemo katika agano la Israeli na Mungu. SIku chache tu baada ya Waisraeli Kutoka Misri, Mungu aliwaahidi hivi:
Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yoyote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye (Kutoka 15:26).
Yeyote aliye mkweli atakubali kwamba uponyaji ulikuwemo katika agano la Mungu na Israeli, kutegemeana na utii wa watu. (Hata Paulo anaweka wazi kabisa katika 1Wakor. 11:27-31) kwamba afya ya kimwili katika agano jipya hutegemeana na utii wetu pia.)
Vile vile, Mungu aliwaahidi Waisraeli hivi:
Nanyi mtamtumikia BWANA Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza (Kutoka 23:25-26. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Utabarikiwa kulio mataifa yote; hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu wala kati ya wanyama wenu wa mifugo. Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yoyote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao (Kumbu. 7:14-15. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Ikiwa uponyaji ulihusishwa katika agano la kale, mtu atashangaa kiwa hautahusishwa katika agano jipya, ikiwa agano jipya ni bora kuliko la zamani kama yanavyosema Maandiko.
Lakini sasa [Yesu] amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora (Waebrania 8:6. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Uthibitisho Zaidi Tena
Biblia ina Maandiko mengi sana yenye kutoa uthibitisho usiopingika kwamba ni mapenzi ya Mungu kumponya kila mtu. Hebu nitaje mistari mitatu iliyo bora zaidi.
Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA. Naama, vyote vilivyo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote (Zaburi 103:1-3. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Ni Mkristo gani atakayepingana na tamko la Daudi kwamba Mungu anapenda kusamehe maovu yetu yote? Ila, Daudi aliaminipia kwmaba Mungu anataka kuponya magonjwa yetu yote.
Mwanangu: sikiliza maneno yangu; tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, na afya ya mwili wao wote (Mithali 4:20-22. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa (Yakobo 5:14-15. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Ona kwamba ahadi hii ya mwisho ni kwa yeyote aliye mgonjwa. Tena, ona kwamba si wazee wala mafuta yanayoleta uponyaji, bali ni “maombi ya imani.”
Je, ni imani ya wazee au ya mgonjwa? Ni imani ya wote wawili. Imani ya mgonjwa inaonyeshwa kwa sehemu anapowaita wazee wa kanisa. Kutokuamini kwa mgonjwa kungeweza kubatilisha matokeo ya maombi ya wazee. Aina hii ya maombi inayosemwa na Yakobo ni mfano mzuri kuhusu “maombi ya makubaliano” ambayo Yesu alitaja katika Mathayo 18:19. Wote wanaohusika katika maombi aina hii lazima “wakubaliane.” Kama mmoja anaamini na mwingine haamini, hawakubaliani.
Pia tunajua kwamba katika vifungu kadhaa, Biblia inamtaja Shetani kama mhusika wa magonjwa (ona Ayubu 2:7; Luka 13:16; Matendo 10:38; 1Wakor. 5:5). Basi, ni sawa kabisa kwamba Mungu apingane na kazi ya Shetani katika miili ya watoto Wake. Baba yetu anatupenda sana kuliko baba yeyote wa duniani anavyoweza kuwapenda watoto wake (ona Mathayo 7:11), nami sijawahi kukutana na baba aliyetamani watoto wake kuwa wagonjwa.
Kila uponyaji wa Yesu wakati wa huduma Yake hapa duniani na kila uponyaji unaotajwa katika kitabu cha Matendo unapaswa kututia moyo kuamini kwamba Mungu anataka sisi tuwe na afya njema. Mara nyingi sana Yesu aliponya watu waliomtafuta ili waponywe, Naye alisema imani yao ilihusika na muujiza wao. Hii inathibitisha kwamba Yesu hakuchagua watu fulani aliotaka kuwaponya. Mtu yeyote mgonjwa angeweza kumjia kwa imani na kuponywa. Alitaka kuwaponya wote, lakini alitaka wawe na imani.
Majibu Kwa Baadhi Ya Hoja Pinzani
Pengine hoja pinzani ya kawaida kabisa kwa hayo yote ni ile itokanayo na mambo waliyopitia watu, bila kuw ana msingi kwenye Neno la Mungu. Mara nyingi inasemekana hivi: “Nilimjua mwanamke mmoja – Mkristo mzuri sana – ambaye aliomba aponywe kensa, lakini akafa. Hii inathibitisha kwamba si mapenzi ya Mungu kuwaponya wote.”
Hatupaswi kamwe kuamua mapenzi ya Mungu kwa kutumia kitu kingine ambacho si Neno Lake. Kw amfano: Kama ungerudi nyuma katika wakati na kuwaona Waisraeli wakitangatanga nyikani kwa miaka arobaini huku nchi ya ahadi iliyojaa maziw ana asali ikisubiri ng’ambo tu ya Mto Yordani, ungedhani kwamba hayakuwa mapenzi ya Mungu kwa Israeli kuingia katika nchi ya ahadi. Lakini kama unaijua Biblia, basi ungetambua kwamba si hivyo. Hakika ilikuwa ni mapenzi ya Mungu kwa Israeli kuingia katika Nchi ya Ahadi, lakini walishindwa kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao wenyewe (ona Waebrania 3:19).
Vipi kuhusu watu wote ambao kwa sasa wako jehanamu? Ulikuwa mpango wa Mungu wao wawe mbinguni, lakini hawakutimiza masharti ya toba na imani katika Bwana Yesu. Vivyo hivyo, hatuwezi kuamua mapenzi ya Mungu kuhusu uponyaji kwa kuwatazama watu wagonjwa. Kwa kuwa Mkristo anaweza kuomba uponyaji na akashindwa kupokea hakumaanishi kwamba si mapenzi ya Mungu kuponya kabisa. Kama huyo Mkristo angetosheleza masharti ya Mungu, angeponywa, la sivyo Mungu ni mwongo. Tunaposhindwa kupokea uponyaji halafu tumlaumu Mungu kwa kusema kwamba uponyaji haukuwa mapenzi Yake, hatuwi na tofauti yoyote na Waisraeli wasioamini waliokufa nyimani wakidai kwamba hayakuwa mapenzi ya Mungu kwao kuingia katika Nchi ya Ahadi. Ni afadhali tumeze mate na kiburi chetu na kukiri kwamba sisi ndiyo wenye matatizo.
Kama tulivyoona katika sura iliyotangulia kuhusu imani, Wakristo wengi wa kweli wamemalizia maombi yao kuhusu uponyaji kimakosa kwa kusema maneno yafuatayo, ambayo yanaharibu imani: “Kama ni mapenzi Yako.” Hii inadhihirisha waziwazi kwamba hawaombi kwa imani kwa sababu hawana uhakika wa mapenzi ya Mungu. Kwa habari ya uponyaji, mapenzi ya Mungu ni wazi kabisa, kama ambavyo tumekwisha ona. Kama unajua Mungu anataka kukuponya, hakuna haja ya kuongeza “Kama ni mapenzi Yako” kwenye hiyo sala yako ya kuponywa. Hiyo ni sawa na kumwambia Mungu hivi: “Bwana, najua uliahidi kuniponya, lakini endapo hukumaanisha hivyo, naomba uniponye kama tu ni mapenzi Yako.”
Pia ni kweli kabisa kwamba Mungu anaweza kuwaadhibu waamini wasiokuwa watii kwa kuruhusu magonjwa yawatese, mpaka kufikia mahali pa kuruhusu kifo chao kabla ya muda wao, mara zingine. Waamini hao wanahitaji kutubu kabla ya kupokea uponyaji (ona 1Wakor. 11:27-32). Kuna wengine pia ambao kwa kutokujali miili yao, wanafungua milango wapate magonjwa. Wakristo wanatakiwa kuwa na akili za kutosha kula chakula chenye kuleta afya, kula kwa kiasi, kufanya mazoezi mara kwa mara, na kupumzika inapotakiwa.
Hoja Pinzani Nyingine
Mara nyingi imesemekana hivi: “Paulo alikuwa na mwiba katika mwili wake, na Mungu hakumponya.”
Wazo kwamba mwiba wa Paulo ulikuwa ugonjwa ni wazo baya tu la kitheolojia, maana Paulo mwenyewe alituambia mwiba huo ulikuwa nini. Ulikuwa malaika wa Shetani.
Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi kwa wingi wa mafunuo hayo, nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajli ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi ili uweza wa Kristo ukae juu yangu (2Wakor. 12:7-9. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Katika Kiyunani, neno mjumbe ni “aggelos,) ambalo linatafsiriwa kuwa malaika katika sehemu zaidi ya 160 katika Agano Jipya. Basi, mwiba wa Paulo mwilini ulikuwa malaika wa Shetani aliyetumwa kumpiga – haukuwa ugonjwa au maradhi.
Onapia kwamba Paulo hakuomba aponywe, wala hakuna dalili kwamba Mungu alikataa kumponya. Mara tatu, Paulo alimwomba Mungu kama angeweza kumwondoa huyo malaika anayempiga, na Mungu akamwambia neema Yake inamtosha.
Ni nani aliyempa Paulo mwiba huu? Kuna wanaoamini kwamba ni Shetani, kwa sababu mwiba wenyewe unaitwa “mjumbe wa Shetani.” Wengine wanaamini ni Mungu kwa sababu mwiba ulitolewa ili Paulo asijivune. Paulo mwenyewe alisema kwamba ni “makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi”.
Tafsiri nyingine iko tofauti kidogo. Badala ya kusema, “makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi” inasema, “nisije nikatukuzwa kupita kiasi.” Kuna tofauti kubwa hapo kwa sababu Mungu hapingi sisi kutukuzwa. Ukweli ni kwamba, ameahidi kututukuza kama tutajinyenyekeza. Basi, inawezekana kabisa kwamba Mungu ndiye aliyekuwa anamtukuza, na Shetani alikuwa anajaribu kuzuia kutukuzwa kwa Paulo kwa kumpangia malaika wa kumpiga ili kusababisha fujo kokote Paulo alikokwenda. Lakini Mungu alisema angetumia mazingira hayo kwa ajili ya utukufu Wake kwa sababu uwezo Wake ungedhihirishwa zaidi katika maisha ya Paulo kwa sababu ya udhaifu wake.
Vyovyote vile – kusema kwamba Paulo alikuwa mgonjwa na Mungu akakataa kumponya ni upotoshaji mkubwa sana wa kinachosemwa na Biblia. Katika fungu kuhusu mwiba katika mwili wake, Paulo hakutaja ugonjwa wowote, na hakuna kinachofanana na Mungu kukataa kumponya ugonjwa wake. Kama mtu mkweli atasoma orodha ya majaribu yake yote katika 2Wakorintho 11:23-30, hatakuta ugonjwa hata mmoja ukitajwa, wala maradhi.
Maelezo Zaidi Juu Ya Mada Hiyo
Kuna wanaopinga maelezo haya kuhusu mwiba wa Paulo, wakisema hivi: “Si Paulo mwenyewe aliwaambia Wagalatia kwamba alikuwa mgonjwa alipowahubiria Injili mara ya kwanza? Je, hapo hakuwa anasema kuhusu mwiba wake katika mwili?”
Yafuatayo ni maneno halisi ya Paulo, aliyoandika katika barua yake kwa Wagalatia.
Lakini mwajua ya kuwa naliwahubiri Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili; na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu (Wagalatia 4:13-14).
Neno la Kiyunani asthenia linalotumika hapa katika Wagalatia 4:13 maana yake ni udhaifu. Linaweza kumaanisha udhaifu kwa sababu ya ugonjwa, lakini si lazima iwe hivyo.
Kwa mfano: Paulo aliandika hivi: “Udhaifu wa Mungu ni nguvu kuliko nguvu za wanadamu” (1Wakor. 1:25, TLR. Maneno mepesi kutilia mkazo). Neno linalotumiwa hapo pia ni asthenia. Kama watafsiri wangetafsiri na kusema hivi: “Ugonjwa wa Mungu una nguvu kuliko nguvu za wanadamu” isingeleta maana yoyote. (Ona pia Mathayo 26:41 na 1Petro 3:7, ambapo neno hilo hilo asthenia linatafsiriwa kuwa ni udhaifu na haliwezi kutafsiriwa ugonjwa).
Paulo alipotembelea Galatia kwa mara ya kwanza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Matendo, hakuna taarifa yoyote ya yeye kuwa mgonjwa. Lakini, tunaambiwa kwamba alipigwa mawe na kuachwa akiwa amekufa. Basi, aidha alifufuliwa kutoka kwa wafu au alipona kimuujiza (ona Matendo 14:5-7, 19-20). Bila shaka mwili wa Paulo ulikuwa katika hali mbaya baada ya kupigwa mawe na kuachwa amekufa. Ulikuwa na michubuko na kukatika-katika sana kila mahali.
Paulo hakuwa na ugonjwa wa aina yoyote huko Galatia, uliokuwa jaribu kwa wasikilizaji wake. Ila, mwili wake ulikuwa dhaifu kutokana na kupigwa kwake mawe. Bila shaka alikuwa na mabakio au alama za kuteswa kwake huko Galatia wakati aliowaandikia barua Wagalatia, maana alimaliza waraka huo kwa maneno yafuatayo:
Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu (Wagalatia 6:17).
Hoja Nyingine: “Ninateseka Kwa Utukufu Wa Mungu”
Hoja hii hutumiwa na baadhi ya watu ambao wamechukua mstari kutoka katika kisa cha kufufuliwa kwa Lazaro na kuufanya msingi wa kudai kwamba wanaugua ugonjwa kwa utukufu wa Mungu. Yesu alisema hivi kumhusu Lazaro:
Ugonjwa huu hautaishia kifoni, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa (Yohana 11:4).
Yesu hakuwa anasema kwamba Mungu alikuwa anatukuzwa kwa sababu ya Lazaro kuwa mgonjwa. Alimaanisha kwamba Mungu angetukuzwa wakati ambapo Lazaro angeponywa na kufufuliwa kutoka kwa wafu. Yaani, mwisho wa ugonjwa huo usingekuwa mauti bali Mungu angetukuzwa. Mungu hatukuzwi katika ugonjwa; anatukuzwa katika uponyaji (ona pia Mathayo 9:8; 15:31; Luka 7:16; 13:13 na 17:15, mahali ambapo uponyaji ulileta utukufu kwa Mungu.)
Hoja Nyingine: “Paulo Alisema Amemwacha Trofimo Akiwa Mgonjwa Huko Mileto”
Maneno haya yanaandikwa katika mji fulani huko Ujerumani. Nilipoondoka nyumbani, niliwaacha watu wengi wakiwa wagonjwa. Niliacha hospitali zimejaa wagonjwa. Hiyo haimaanishi kwamba hayakuwa mapenzi ya Mungu kwa wote kuponywa. Kwa kuwa Paulo aliacha mtu mmoja tu mgonjwa katika mji aliotembelea si ushahidi kwamba hayakuwa mapenzi ya Mungu kwa mtu huyo kuponywa. Vipi kuhusu makundi ya watu wasio-okoka ambayo Paulo aliyaacha pia? Je, inathibitisha kwamba hayakuwa mapenzi ya Mungu kwao kuokoka? La sivyo, hata kidogo.
Hoja Nyingine: “Mimi Ni Kama Ayubu!”
Bwana Asifiwe! Kama umesoma mwisho wa habari za Ayubu, unajua kwamba aliponywa. Hayakuwa mapenzi ya Mungu kwamba Ayubu aendelee kuwa mgonjwa, na si mapenzi ya Mungu kwako pia kuendelea kuwa mgonjwa. Habari za Ayubu zinatilia mkazo kwamba mapenzi ya Mungu sikuzote ni kuponya.
Hoja Nyingine: Ushauri Wa Paulo Kwa Timotheo Kuhusu Tumbo Lake
Tunajua kwamba Paulo alimwambia Timotheo atumie mvinyo kidogo kwa ajili ya tumbo lake, na magonjwa yake ya mara kwa mara (ona 1Timo. 5:23).
Ukweli ni kwamba Paulo alimwambia Timotheo aache kunywa maji na atumie mvinyo kidogo kwa ajili ya tumbo lake, na magonjwa ya mara kwa mara. Hii inaonyeha kwamba maji yalikuwa na matatizo fulani. Ni hivi: Kama unakunywa maji machafu, acha kuyanywa uanze kunywa kitu kingine, la sivyo utakuwa na matatizo ya tumbo kama Timotheo.
Hoja Nyingine: “Yesu Aliponya Ili Kuthibitisha Uungu Wake Tu”
Watu wengine wanataka tuamini kwamba sababu ya pekee ya Yesu kuponya ilikuwa kuthibitisha Uungu Wake. Kwa vile Uungu Wake umethibitishwa vizuri kabisa, inasemekana haponyi tena.
Hayo ni makosa kabisa. Ni kweli kwamba miujiza ya Yesu ilihalalisha Uungu Wake, lakini hiyo si sababu ya pekee iliyomfanya aponye watu wakati wa huduma Yake hapa duniani. Mara nyingi sana aliwaambia watu aliowaponya wasimwambie yeyote mambo yaliyokuwa yametokea kwao (ona Mathayo 8:4; 9:6, 30; 12:13-16; Marko 5:43; 7:36; 8:26). Ikiwa Yesu aliwaponya watu kwa kusudi moja tu la kuthibitisha Uungu Wake, angewaambia watu hao kumwambia kila mtu yale aliyokuwa amewatendea.
Nini kilichokuwa nyuma ya matendo ya kuponya yaliyofanywa na Yesu? Mar anyingi Maandiko yanasema aliponya kwa sababu “aliwahurumia watu” (ona Mathayo 9:35-36; 14:14; 20:34; Marko 1:41; 5:19; Luka 7:13). Yesu aliponya watu kwa sababu aliwapenda na alikuwa amejaa huruma. Je, Yesu amepunguza huruma baada ya huduma Yake ya hapa duniani? Je, upendo Wake umepungua? Hapana hata kidogo!
Hoja Nyingine: “Mungu Anataka Niwe Mgonjwa Kwa Sababu Fulani”
Hiyo haiwezekani kwa sababu ya Maandiko yote tuliyokwisha angalia. Kama wewe umedumu katika kutokutii, yawezekana ni kweli kwamba Mungu ameruhusu ugonjwa wako ili akufikishe kwenye toba. Lakini, bado si mapenzi Yake kwamba ubakie mgonjwa. Anataka utubu na kuponywa.
Tena, kama Mungu anataka uwe mgonjwa, mbona unakwenda kwa daktari na kupokea dawa, ukitazamia kuponywa? Kwani unajaribu kuepuka “mapenzi ya Mungu”?
Hoja Ya Mwisho: “Tusipopata Magonjwa, Tutakufaje?”
Tunajua Biblia inafundisha kwamba miili yetu inachakaa (ona 2Wakor. 4:16). Hakuna tunachoweza kufanya kuzuia nywele zetu kuwa na mvi, na miili yetu kuzeeka. Mwishoni, hatu taweza kuona vizuri wala kusikia vizuri kama ilivyokuwa tukiwa vijana. Hatuwezi kukimbia. Mioyo yetu haiwi na nguvu sana. Tunachakaa pole pole.
Lakini haimaanishi kwamba lazima tufe kwa ugonjwa au maradhi. Miili yetu inaweza kuchoka kabisa, na ikifikia hapo, roho zetu zitaiacha miili yetu Mungu atakapotuita nyumbani huko mbinguni. Waamini wengi wamekufa katika hali hiyo. Mbona na wewe isiwe hivyo kwako?
[1] Katika makanisa mengine ya Marekani, mchungaji akifundisha somo hili atakuwa anajihatarisha sana kwa sababu ya upinzani mkubwa ambao angepata kutoka kwa wanaojiita waamini. Hata Yesu alikutana na upinzani na kutokuamini wakati mwingine, vitu vilivyozuia huduma Yake ya kuponya (ona Marko 6:1-6).
[2] Katika kushika chochote kitakachowawezesha kuunga mkono kutokuamini kwao, wengine hujaribu kutushawishi kwamba Yesu alitimiza kabisa Isaya 53:4 kwa kuwaponya watu kadhaa jioni ile pale Kapernaumu. Lakini, Isaya alisema kwamba Yesu aliyachukua magonjwa yetu, sawa tu na alivyosema kwamba Yesu alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu (lingansiha Isaya 53:4 na 5). Yesu alichukua magonjwa ya watu wengi kama wale ambao maovu yao yalimfanya achubuliwe. Kwa hiyo, Mathayo alikuwa anaonyesha tu kwamba huduma ya Yesu ya kuponya pale Kapernaumu ilithibitisha kwamba alikuwa ndiye Masiya anayetajwa katika Isaya 53, yeye ambaye angeyachukua magonjwa yetu na maradhi yenye kutusumbua.
[3] Kwa mfano: Yesu alimwambia mwanamke aliyekuwa amemponya kutokwa damu, “Binti, imani yako imekuponya” (Marko 5:34, TLR). Neno la Kiyunani linalotumika kusema “imekuponya” katika mstari huu (sozo) na katika sehemu zingine kumi katika Agano Jipya lina maana ya “kuokoa” au “okoa” na linatumika zaidi ya mara themanini katika Agano Jipya. Kwa mfano, ndiyo neno linalotumiwa kusema “kuokoa” katika Waefeso 2:5, hivi: “Kwa neema ninyi mmeokolewa kwa njia ya imani.” Ni kwamba uponyaji wa kimwili upo katika mantiki ya neno la Kiyunani linalotumiwa mara nyingi kusema kuhusu “kuokoka.”