Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo … Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo (Waefeso 4:7, 11-13. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha (1Wakor. 12:28. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Karama za huduma kama zinavyojulikana, ni tendo la kuitwa kwa waamini fulani na kupewa uwezo ili kusimama katika nafasi kama mtume, nabii, mwinjilisti, mchungaji au mwalimu. Hakuna mtu awezaye kujiweka katika nafasi hizo. Ni lazima mtu aitwe na apewe karama hiyo na Mungu.
Inawezekana kwa mtu mmoja kushika nafasi zaidi ya moja kati ya hizo, lakini ni kwa makundi fulani fulani. Kwa mfano: Inawezekana mwamini mmoja akaitwa kushika nafasi ya mchungaji na mwalimu, au nabii na mawalimu. Lakini si rahisi kwa mtu kuitwa kushika nafasi ya mchungaji na mwinjilisti kwa sababu, huduma ya mchungaji inadai kwamba abaki mahali pamoja akihudumia kusanyiko la mahali pamoja. Hivyo, asingeweza kutimiza wito wa uinjilisti ambao unadai mtu kusafiri mara kwa mara.
Japo hizo nafasi tano zote ni karama tofauti kwa makusudi tofauti, zimetolewa kwa kanisa kwa kusudi moja kubwa la jumla – kuwawezesha watakatifu kwa ajili ya kazi ya huduma” (Waefeso 4:12, TLR).[1] Lengo la kila mtumishi linapaswa kuwa kuwawezesha watakatifu kwa ajili ya kufanya huduma. Lakini, mara nyingi, wale walio katika huduma hujifanya kana kwamba wameitwa kuwastarehesha watu wa kimwili wanaofika kanisani – si kuwawezesha watakatifu kuwa tayari kwa huduma. Kila mtua liyeitwa katika nafasi mojawapo kati ya hizo zilizotajwa anapaswa kutathmini mara kwa mara mchango anaotoa kwa habari ya “kuwawezesha watakatifu kwa ajili ya kufanya huduma”. Kama kila mtumishi angefanya hivyo, wengi wangeondoa shughuli nyingi mbalimbali ambazo zinahesabiwa kwa sasa kwamba ni “huduma”.
Je, Karama Zingine Za Huduma Zilikuwa Kwa Ajili Ya Kanisa La Mwanzo Tu?
Je, karama hizi za huduma zitatolewa kwa kanisa kwa muda gani? Yesu atatizoa kwa muda wote ambapo watakatifu Wake wanahitaji kuwezeshwa kufanya huduma. Hiyo ni mpaka atakaporudi. Kila mara kanisa linapokea Wakristo waliozaliwa upya wanaohitaji kukua, na sisi wengine tunahitaji kuendelea kukua na kukomaa kiroho daima.
Kwa bahati mbaya, kuna wengine ambao wamedhani kwamba kuna aina mbili tu ya huduma siku hizi – wachungaji na wainjilisti – kana kwamba Mungu amebadilisha mpango Wake. Hapana! Bado tunahitaji mitume, manabii na waalimu, kama kanisa la mwanzo lilivyohitaji. Sababu ya kutokuona mifano ya karama hizi katika kanisa kwa wingi duniani ni kwamba, Yesu ndiye anayetoa karama hizo kwa Kanisa Lake, si hli kanisa la siku hizi la bandia, lisilokuwa takatifu, lenye kuhubiri injili za uongo. Katika kanisa hili bandia utawapata wale wanaojitahidi – kwa unyonge sana – kujaza nafasi za baadhi ya karama za huduma (sana sana wachungaji na wainjilisti wachache tu), lakini hawafanani hata kidogo na zile karama za huduma ambazo zinatolewa na Mungu, ambazo Yesu hutoa kwa kanisa Lake. Tena, hawawawezeshi watakatifu kufanya matendo ya huduma, kwa sababu injili yenyewe wanayotangaza haileti utakatifu bali huwadanganya watu wafikiri tu kwamba wamesamehewa. Na hao watu hawana haja ya kuwezeshwa wafanye huduma. Hawana nia ya kujikana wenyewe na kuibeba misalaba yao.
Utajuaje Kwamba Umeitwa?
Mtu anajuaje kwamba ameitwa kushika mojawapo ya nafasi hizo kanisani? Kwanza kabisa, atasikia mwito kutoka kwa Mungu. Atajikuta ana mzigo wa kutenda kazi fulani. Hii ni zaidi ya kuwa na haja ya kuona hitaji ambalo linaweza kutimizwa. Badala yake, ni njaa itokayo kwa Mungu, iliyoko ndani, yenye kumsukuma mtu kuingia katika huduma fulani. Kama kweli ameitwa na Mungu, hatatosheka mpaka aanze kutimiza wito wake. Wala haihusiani na watu kumchagua au kamati ya watu. Mungu ndiye anayeita.
Pili – Mtu aliyeitwa kweli atajikuta amewezeshwa na Mungu ili kutimiza kazi hiyo aliyopewa na Mungu. Kila nafasi katika zile tano ina upako wake wa KiMungu, wenye kumwezesha mhusika kufanya kile ambacho Mungu amemwita kufanya. Upako huja pamoja na mwito wenyewe. Kama hakuna upako, hakuna mwito. Mtu anaweza kutamani kufanya kazi katika huduma fulani, akaenda Shule ya Biblia kwa miaka minne kujifunza na kujiandaa kwa ajili ya huduma hiyo, lakini pasipo upako toka kwa Mungu, hana nafasi ya kufanikiwa.
Tatu – Ataona Mungu akifungua mlango au nafasi kwa ajili ya kufanyia kazi karama zake hizo. Kwa hali hiyo anaweza kujithibitisha kuwa mwaminifu, na hatimaye atapewa nafasi kubwa zaidi, majukumu makubwa zaidi na karama zaidi.
Kama mtu hajasikia mwito wa Mungu au msukumo wa ndani kuhusiana na mojawpao ya hizo karama tano za huduma, au kama hajisikii upako maalum wa aina yoyote ile ili kutekeleza kazi itolewayo na Mungu, au kama hakuna nafasi iliyojitokeza kutumia karama anayofikiri anayo, basi asijaribu kuwa kitu ambacho Mungu hajamwita kuwa. Badala yake, afanye bidii kuwa baraka katika kusanyiko lake, katika mahali anapokaa na kazini anakofanya. Hata ingawa hajaitwa kwenye “huduma tano” hizo, ameitwa kutumika kwa kufanyia kazi zile karama ambazo Mungu amempa, na anatakiwa ajithibitishe kuwa ni mwaminifu.
Ingawa Maandiko yanataja hizo karama tano za huduma, hii haimaanishi kwamba kila mtu anayeshika nafasi fulani atakuwa na huduma inayofanana na mwingine. Paulo aliandika kwamba kuna “tofauti za huduma” (1Wakor. 12:5), akionyesha uwezekano wa kutofautiana kati ya watumishi wanaoshikilia nafasi zinazofanana. Tena, inaonekana kuna viwango mbalimbali vya upako juu ya hao wanaoshikilia nafasi hizo. Basi, tunaweza kutofautisha kila nafasi kwa kiwango cha upako. Kw amfano: Kuna waalimu ambao wanaonekana kuwa na upako zaidi kuliko wengine. Ndivyo ilivyo hata katika karama zingine za huduma. Mimi ninaamini kwamba mtumishi yeyote anaweza kufanya mambo yatakayosababisha ongezeko la upako juu ya huduma yake, kama kuwa mwaminifu na kujitolea sana kwa Mungu.
Tutazame Kwa Karibu Nafasi Ya Mtume
Neno la Kiyunani linalotafsiriwa mtume ni apostolos na maana yake halisi ni “aliyetumwa”. Mtume wa kweli wa Agano Jipya ni mwamini anayetumwa na Mungu kwenda mahali fulani au maeneo fulani ili kuanzisha makanisa. Anaweka msingi wa kiroho wa “jengo” la Mungu, na anafananishwa na fundi ujenzi mkandarasi. Paulo, yeye mwenyewe akiwa mtume, aliandika hivi:
Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu. Ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi kama mkuu wa wajenzi wenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake (1Wakor. 3:9-10a. Maneno mepesi kutilia mkazo).
“Mkuu wa wajenzi” husimamia mpango mzima wa kujenga – yeye anaona jengo lililokamilika. Si mtaalamu kama vile fundi seremala au mwashi. Anaweza kuwa na uwezo wa kufanya kazi ya fundi seremala au mwashi, lakini pengine hataifanya vizuri kama wao wenyewe. Vivyo hivyo, mtume anao uwezo wa kufanya kazi ya mwinjilisti au mchungaji, lakini kwa muda tu wakati anapoanzisha makanisa. (Mtume Paulo kwa kawaida alikuwa anakaa mahali kwa miezi sita hadi miaka mitatu.)
Mtume anafaa sana kuanzisha makanisa, kisha kuyasimamia ili kuhakikisha yanaendelea kama Mungu anavyotaka. Mtume anawajibika kuweka wazee au wachungaji au wasimamizi ili kuchunga kila kundi analoanzisha (ona Matendo 14:21-23; Tito 1:5).
Mitume Wa Kweli Na Wa Uongo
Inaonekana kwamba baadhi ya watumishi siku hizi, kwa kutamani kuwa na madaraka juu ya makanisa, ni wepesi kujitangaza kwamba wameitwa kuwa mitume. Lakini wengi wao wana matatizo makubwa. Kwa kuwa hawajaanzisha makanisa (au labda wana moja au mawili) na hawana karama wala upako wa kiBiblia wa utume, inawabidi watafute wachungaji wepesi kudanganyika watakaowaruhusu wao kuwa na mamlaka juu ya makanisa yao. Kama wewe ni mchungaji, usidanganywe na hao mitume wa uongo wenye kujitukuza wenyewe na wenye njaa ya mamlaka. Wao kwa kawaida ni mbwa mwitu waliovaa mavazi ya kondoo. Mara nyingi wanachotafuta ni fedha tu. Maandiko yanaonya kuhusu mitume wa uongo (ona 2Wakor. 11:13; Ufunuo 2:2). Kama inabidi wakwambie wao ni mitume, basi ni ishara kwamba wao si mitume. Matunda yao yanapaswa kuzungumza.
Mchungaji anayeanzisha kanisa na kuendelea kulichunga kama mchungaji kwa miaka mingi si mtume. Pengine wachungaji aina hiyo wanaweza kuitwa “wachungaji wa kitume” kwa kuwa walianzisha makanisa wenyewe. Pamoja na hayo, wasishike nafasi ya mtume kwa sababu mtume huendelea kuanzisha makanisa.
“Mishenari” aliyetumwa kweli na Mungu na kutiwa mafuta – ambalo ndilo jina la mitume siku hizi – mwenye wito wa kuanzisha makanisa, anaweza kusimama kama mtume. Lakini, wamishenari wanaofanya kazi ya kuanzisha shule za Biblia au kuwafundisha wachungaji si mitume bali waalimu.
Huduma ya kweli ya mtume huonekana kwa ishara na maajabu, ambavyo ni vyombo vinavyosaidia kuanzisha kanisa. Paulo aliandika hivi:
Kwa sababu sikuwa duni ya mtume walio wakuu kwa lolote, nijapokuwa si kitu. Kweli ishara za mtume zilitendwa katikati yenu katika saburi yote, kwa ishara na maajabu na miujiza (2Wakor. 12:11b-12).
Kama mtu hana ishara na maajabu katika huduma yake, yeye si mtume. Basi, mitume wa kweli si wengi, na hawapatikani katika kanisa bandia, lisilo takatifu, lenye kuhubiri injili bandia. Sana sana wanapatikana katika maeneo mapya kabisa duniani ambayo hajapata Injili bado.
Cheo Cha Juu Cha Mtume
Katika orodha zote za karama za huduma katika Agano Jipya, nafasi ya mtume hutajwa kwanza, kuonyesha kwamba ndiyo wito wa hali ya juu zaidi (ona Waefeso 4:11; 1Wakor. 12:28).
Hakuna mtu aanzaye huduma yake kama mtume. Mtu anaweza kuwa na wito wa mtume, lakini hataanza katika nafasi hiyo. Ni lazima kwanza ajithibitishe kuwa mwaminifu kwa miaka mingi katika kuhubiri na kufundisha, kisha hatimaye atasimama katika nafasi ambayo Mungu amemwandalia. Paulo aliitwa kuwa mtume toka tumboni mwa mama yake, lakini alifanya huduma kwa miaka mingi kabla ya kuingia katika nafasi hiyo hatimaye (ona Wagalatia 1:15 – 2:1). Alianza kama mwalimu na nabii (ona Matendo 13:1-2), ndipo baadaye akapandishwa cheo na kuwa mtume, wakati alipotumwa na Roho Mtakatifu (ona Matendo 14:14).
Tunaona wengine wakitajwa kama mitume licha ya Paulo na wale Thenashara, katika Matendo 1:15-26; 14:14; Warumi 16:7; 2Wakor. 8:23; Wagalatia 1:17-19; Wafilipi 2:25 na 1Wathes. 1:1 na 2:6. (Neno mtenda kazi katika 2Wakor. 8:23 na Wafilipi 2:25 katika Kiyunani ni apostolos.) Hii hupingana na dhana iliyoko siku hizi kwamba nafasi ya mtume ilikuwa kwa ajili ya watu kumi na mbili tu.
Ila, ni mitume kumi na mbili tu wanaoweza kuhesabiwa kuwa “Mitume wa Mwanakondoo,” na ni hao kumi na mbili tu ndiyo watakaokuwa na nafasi ya pekee katika utawala wa Kristo wa miaka elfu moja (tazama Mathayo 19:28; Ufunuo 21:14). Hatuhitaji tena mitume kama Petro, Yakobo na Yohana ambao walivuviwa kipekee ili kuandika Maandiko, kwa sababu ufunuo wa Biblia umekamilika. Ila, sku hizi bado tunahitaji mitume watakaoanzisha makanisa kwa nguvu za Roho Mtakatifu, kama walivyofanya akina Paulo na wengine, kulingana na tunavyosoma katika Kitabu cha Matendo ya Mitume.
Nafasi Ya Nabii
Nabii ni mtu anayepokea mafunuo ya Mungu na kusema kwa upako wa Mungu. Kwa kawaida, anatumiwa mara kwa mara katika karama ya kiroho ya unabii pamoja na zile karama za ufunuo: neno la hekima, neno la maarifa, na kupambanua roho.
Mwamini yeyote anaweza kutumiwa na Mungu katika karama ya unabii kama apendavyo Roho, lakini hiyo haimfanyi kuwa nabii. Nabii kwanza kabisa ni mtumishi anayeweza kuhubiri au kufundisha kwa upako. Kwa kuwa nafasi ya nabii inaonekana kuwa mwito wa pili (ona orodha katika 1Wakor. 12:28), hata mtumishi wa kudumu asingeweza kutiwa katika nafasi ya nabii mpaka awe katika huduma kwa miaka kadhaa. Inapofikia wakati wake kushika nafasi hiyo, atakuwa na vitendea kazi vya kiroho vinavyoambatana na nafasi yenyewe.
Watu wawili wanaotajwa katika Agano Jipya kuwa manabii ni Yuda na Sila. Tunasoma katika Matendo 15:32 kwamba walitoa unabii mrefu kwa kanisa la Antiokia, kama ifuatavyo:
Tena Yuda na Sila, kwa kuwa wao wenyewe ni manabii, wakawausia ndugu kwa maneno mengi, wakawathibitisha.
Mfano mwingine wa nabii kutoka katika Agano Jipya ni Agabo. Tunasoma hivi katika Matendo 11:27-28:
Siku zizo hizo manabii walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia. Na tulipokusanyika, akasimama mmoja wao jina lake Agabo, akaonyesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio.
Ona kwamba Agabo alipewa neno la hekima – kitu kuhusu wakati ujao kilifunuliwa kwake. Agabo hakujua kila kitu ambacho kingetokea katika siku zijazo, ila alifahamu yale tu ambayo Roho Mtakatifu alipenda kumfunulia.
Katika Matendo 21:10-11, kuna mfano mwingine wa neno la hekima kufanya kazi katika huduma ya Agabo. Hapa, ilitokea kwa ajili ya mtu mmoja, Paulo.
Basi, tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia, akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, “Roho Mtakatifu asema hivi, ‘Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa’.”
Je, Maandiko yanaruhusu katika kipindi hiki cha agano jipya kutafuta ushauri binasi kutoka kwa manabii? Hapana. Sababu ni hii: Waamini wote wana Roho Mtakatifu ndani yao ili kuwaongoza. Nabii anachoweza kufanya ni kuthibitisha tu kile ambacho mwamini tayari anajua ni mwongozo wa Mungu katika roho yake. Kwa mfano: Wakati Agabo alipomtabiria Paulo, hakumpa mwongozo kwamba afanye nini. Alithibitisha tu kile ambacho Paulo alikwisha fahamu kwa muda mrefu.
Kama tulivyokwisha kusema mapema, Paulo alishika nafasi ya nabii (na mwalimu) kabla ya kuitwa katika huduma ya utume (ona Matendo 13:1). Tunajua Paulo alipokea mafunuo kutoka kwa Bwana kulingana na Wagalatia 1:11-12, na pia alipata maono mengi tu (ona Matendo 9:1-9; 18:9, 10; 22:17-21; 23:11; 2Wakor. 12:1-4).
Kama ilivyo kwa habari ya mitume wa kweli, hatupati manabii wa kweli katika kanisa la uongo. Kanisa la uongo huwaepuka manabii wa kweli kama Sila, Yuda au Agabo. Sababu ni kwamba manabii wa kweli wataleta ufunuo wa Mungu kutopendezwa na kutokutii kwao (kama Yohana alivyofanya kwa makanisa mengi ya Asia Ndogo katika sura mbili za kwanza za Ufunuo). Kanisa la uongo halipendi hayo.
Nafasi Ya Mwalimu
Kulingana na orodha ya 1Wakorintho 12:28, nafasi ya mwalimu ni ya tatu. Mwalimu ni mtu ambaye ametiwa mafuta na Mungu kufundisha Neno la Mungu. Si kwamba kila mtu anayefundisha Biblia ni mwalimu kulingana na Agano Jipya. Wengi hufundisha kwa sababu wanajisikia kupenda kufanya hivyo, au wanajisikia kuwajibika kufanya hivyo, lakini mtu ambaye ana wito wa nafasi hiyo ya ualimu hupewa karama na Mungu kwa ajili ya kufundisha. Mara nyingi anapewa ufunuo wa Mungu kuhusu Neno la Mungu, naye anakuwa na uwezo wa kueleza Biblia kwa njia inayofanya ieleweke na kufanyiwa kazi.
Apolo ni mfano wa mtu aliyeshika nafasi hiyo katika Agano Jipya. Paulo alilinganisha huduma yake ya kitume na huduma ya Apolo ya kufundisha katika 1Wakorintho kwa kusema hivi:
Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. … Naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake (1Wakor. 3:6, 10b. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Mwalimu Apolo hakupanda wala kuweka msingi. Ila, yeye alitia maji mimea mipya kwa Neno la Mungu, na alijenga kuta kwenye msingi uliokuwepo.
Anatajwa tena katika Matendo 18:27, hivi:
Na [Apolo] alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.
Ona kwamba Apolo “akawasaidia sana” watu ambao walikuwa Wakristo tayari, na kwamba mafundisho yake yanaelezwa kuwa na nguvu. Mafundisho yenye upako kila wakati yana nguvu.
Huduma ya kufundisha ni ya muhimu sana kwa kanisa kuliko hata matendo ya miujiza au karama za kuponya. Hii ndiyo sababu imeorodheshwa kabla ya karama hizo katika 1Wakorintho 12:28.
Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa (Maneno mepesi kukazia).
Kwa bahati mbaya sana, waaminio wakati mwingine huvutiwa zaidi kuona uponyaji kuliko kusikiliza mafundisho dhahiri ya Neno ambalo litaleta kukua kiroho na utakatifu katika maisha yao.
Biblia inazungumza juu ya kuhubiri na kufundisha. Kufundisha ni kitu cha utaratibu na mpango, ila kuhubiri ni kitu cha uvuvio zaidi. Mara nyingi wainjilisti huhubiri. Waalimu na wachungaji mara nyingi hufundisha. Mitume huhubiri na kufundisha. Ni kitu cha kuhuzunisha kwamba waamini wengine hawatambui thamani ya mafundisho. Wengine hata hufikiri kwamba wakati pekee ambapo msemaji amepokea upako ni wakati wanahubiri kwa sauti kubwa na kwa mwendo wa haraka! Sivyo.
Yesu ni mfano bora kabisa wa mwalimu aliye na upako. Mafundisho Yake yalikuwa na sehemu kubwa sana katika huduma Yake kiasi cha watu wengi kumwita “Mwalimu” (Mathayo 8:19; Marko 5:35; Yohana 11:28).
Kwa maelezo zaidi kuhusu waalimu na kufundisha, ona Matendo 2:42; 5:21, 25, 28, 42; 11:22-26; 13:1; 15:35; 18:11; 20:18-20; 28:30, 31; Warumi 12:6, 7; 1Wakor. 4:17; Wagalatia 6:6; Wakolosai 1:28; 1Timo. 4:11-16; 5:17; 6:2; 2Timo. 1:11; 2:2 na Yakobo 3:1. Andiko la mwisho katika orodha hii linatuambia kwamba waalimu watapata hukumu kali zaidi, kwa hiyo wanapaswa kuwa makini sana kuhusu kitu wanachofundisha. Wanapaswa kufundisha Neno tu.
Nafasi Ya Mwinjilisti
Mwinjilisti ni mtu aliyetiwa mafuta kuhubiri Injili. Jumbe zake zimepangwa kuwaongoza watu watubu na kumwamini Bwana Yesu Kristo. Zinaambatana na miujiza yenye kuvuta usikivu wa wasioamini na kuwafanya kuamini ukweli wa ujumbe wake.
Bila shaka walikuwepo wainjilisti wengi sana katika kanisa la kwanza, lakini ni mtu mmoja tu anayetajwa katika kitabu cha Matendo kama mwinjilisti. Jina lake ni Filipo. Tunasoma hivi: “…Tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake” (Matendo 21:8. Maneno mepesi kukazia).
Filipo alianza huduma yake kama mtumishi tu (au tuseme, “shemasi”) ambaye kazi yake ilikuwa kusimamia meza (ona Matendo 6:1-6). Akapandishwa kufikia nafasi ya mwinjilisti wakati wa mateso ya kanisa yaliyotokana na kuuawa kwa Stefano. Kwa mara ya kwanza alihubiri Injili huko Samaria.
Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule (Matendo 8:5-8).
Ona kwamba ujumbe wa Filipo ulikuwa mmoja tu – Kristo. Lengo lake lilikuwa kuanza kufanya watu kuwa wanafunzi, yaani, wafuasi watiifu wa Kristo. Basi, alimtangaza Kristo kama mtenda miujiza, Mwana wa Mungu, Bwana, Mwokozi na Hakimu anayerudi upesi. Akawashauri watu watubu na kumfuata Bwana wake.
Ona pia kwamba Filipo aliwezeshwa kwa ishara na maajabu, vilivyothibitisha ujumbe wake. Mtu anayesimama katika nafasi ya mwinjilisti atatiwa mafuta kwa karama za kuponya na zingine za kiroho. Kanisa la uongo lina wainjilisti wa uongo ambao wanahubiri injili ya uongo. Dunia imejaa wainjilisti wa namna hiyo, na ni dhahiri kwmaba Mungu hathibitishi mahubiri yao kwa miujiza na uponyaji. Sababu ni kwamba hawahubiri Injili Yake. Hawamhubiri Kristo. Kwa kawaida, wanahubiri kuhusu mahitaji ya watu na jinsi Kristo anavyoweza kuwapa uzima tele, au wanahubiri mfumo wa wokovu ambao hautaki toba. Wanawaongoza watu katika uongofu bandia wenye kupooza hatia yao bila kuwaokoa. Matokeo ya mahubiri yao ni kwamba watu hata hawana nafasi za kuzaliwa mara ya pili, kwa sababu hawaoni haja ya kupokea kitu ambacho wanafikiri wanacho tayari. Wainjilisti aina hiyo wanamsaidia Shetani kujenga ufalme wake.
Nafasi ya mwinjilisti haiko kwenye ile orodha ya karama zingine za huduma katika 1Wakorintho 12:28, kama inavyotajwa katika Waefeso 4:11. Ila, kwa kuwa inatajwa “miujiza na karama za kuponya”, hizo zinahusika na nafasi ya mwinjilisti kwa sababu zilikuwa kawaida katika huduma ya uinjilisti ya Filipo, nazo zinatoa uthibitisho wa Mungu kwenye huduma yoyote ya mwinjilisti.
Wengi wanaotembea kutoka kanisa hadi kanisa na kujiita wainjilisti si wainjilisti kweli kwa sababu wanahubiri katika makanisa, tena kwa Wakristo. Kisha hawana ule uwezo wa karama za kuponya wala miujiza. (Kuna wanaojifanya kuwa na karama hizo, lakini wanawadanganya wajinga tu. Miujiza yao mikubwa ni kuwaangusha watu, tena kwa kuwasukuma.) Hao watumishi wanaosafiri wanaweza kuwa waalimu au wahubiri au wenye kuonya (ona Warumi 12:8), lakini hawako kwenye nafasi ya mwinjilisti. Ila, inawezekana Mungu kuanza huduma ya mtu kwa kumfanya mwonyaji au mhubiri na baadaye kumpandisha hadi nafasi ya mwinjilisti.
Kwa maelezo zaidi kuhusu nafasi ya mwinjilisti, soma Matendo 8:4 – 40, ambayo ni taarifa ya huduma ya Filipo. Ona hapo jinsi karama za huduma zinavyotegemeana na umuhimu wake (hasa mstari wa 14 hadi 25) na jinsi Filipo alivyohubiri Injili kwa watu lakini pia akaongozwa na Mungu kuwahudumia watu binafsi (ona Matendo 8:25-39).
Inaonekana kwamba wainjilisti wameagizwa kuwabatiza waongofu wao, lakini hawajapewa agizo la kutoa ubatizo wa Roho Mtakatifu kwa waamini wapya. Hilo kimsingi ni jukumu la mitume au wachungaji/wazee/waangalizi.
Nafasi Ya Mchungaji
Tumeona katika sura mbili zilizopita mlinganisho kati ya nafasi ya mchungaji KiBiblia na jinsi ilivyo kwa kawaida. Ila, kuna mengine tena ya kusema juu ya huduma ya mchungaji.
Ili kuelewa vizuri kile ambacho Biblia inafundisha kuhusu nafasi ya mchungaji, tunahitaji kuelewa maneno matatu muhimu sana ya Kiyunani. Hayo ni (1) poimen, (2) presbuteros na (3) episkopos. Yanatafsiriwa hivi: (1) mchungaji wa mifugo au mchungaji wa watu, (2) mzee, na (3) mwangalizi au askofu.
Neno poimen linapatikana mara kumi na nane katika Agano Jipya, nalo linatafsiriwa mchungaji wa mifugo mara kumi na saba, na mchungaji wa watu mara moja. Neno lenyewe kama kitendo – poimaino – linapatikana mara kumi na moja, na mara nyingi linatafsiriwa mchungaji wa mifugo.
Neno presbuteros linapatikana mara sitini na sita katika Agano Jipya. Mara sitini limetafsiriwa mzee au wazee.
Neno episkopos linapatikana mara tano katika Agano Jipya, na linatafsiriwa mwangalizi mara nne. Biblia yetu ya Kiswahili inatumia neno askofu.
Hayo maneno yote matatu yanataja nafasi moja katika kanisa, nayo yanatumika kwa kubadilishana. Popote ambapo mtume Paulo alianzisha makanisa, aliweka wazee (presbuteros) ambao waliwaacha kushughulika na makanisa yamahali (ona Matendo 14:23; Tito 1:5). Majukumu yao yalikuwa kusimamia (episkopos) na kuchunga (poimaino) makundi yao. Angalia mfano katika Matendo 20:17, kama ifuatavyo:
Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee [presbuteros] wa kanisa (Maneno mepesi kukazia).
Je, aliwaambia nini hao wazee wa kanisa?
Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi [episkopos] ndani yake, mpate kulilisha [poimaino] kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe (Matendo 20:28. Maneno mepesi kukazia).
Ona jinsi hayo maneno matatu yanavyotumika kwa kubadilishana. Si nafasi tatu tofauti. Paulo aliwaambia wazee kwamba wao ni wasimamizi au waangalizi ambao walipaswa kufanya huduma yao kama wachungaji.
Petro naye aliandika hivi katika waraka wake wa kwanza:
Nawasihi wazee [presbuteros] walio kwenu, mimi niliye mzee mwenzi wao na shahidi wa mateso ya Kristo na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni [poimaino] kundi la Mungu lililo kwenu na kulisimamia, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka (1Petro 5:1-4. Maneno mepesi kukazia).
Petro aliwaambia wazee wawe wachungaji kwa makundi yao. Kitendo hapa kinachotafsiriwa mchungaji kinatumiwa kama jina katika Waefeso 4:11.
Naye [Yesu] alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu (Maneno mepesi kukazia).
Hilo linatufanya tuamini kwamba wazee na wachungaji ni kitu kimoja.
Pia, Paulo alitumia neno mzee (presbuteros) na mwangalizi au askofu (episkopos) kwa kubadilishana, katika Tito 1:5-7.
Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru. … Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshtakiwa neno (Maneno mepesi kukazia).
Hivyo, si rahisi kujenga hoja kwamba nafasi ya mchungaji, mzee na mwangalizi ni tatu tofauti. Basi, chochote kilichoandikwa kuhusu wasimamizi na wazee katika nyaraka za Agano Jipya kinawahusu na wachungaji pia.
Utawala Kanisani
Pia ni dhahiri kabia kutokana na maandiko yaliyotajwa hapo nyuma kwamba, wazee/wachungaji/waangalizi hawajapewa usimamizi wa kiroho tu kwa kanisa, bali pia wamepwa mamlaka ya kutawala. Yaani, wazee/wachungaji/waangalizi ndiyo wasimamizi na wenye mamlaka, na washirika wanapaswa kuwatii.
Watiini wenye kuwaongoza na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu (Waebrania 13:17).
Lakini, hakuna Mkristo anayetakiwa kumtii na kumnyenyekea mchungaji ambaye si mtii wala mnyenyekevu kwa Mungu, bali anapaswa kutambua kwamba hakuna mchungaji aliye mkamilifu.
Wachungaji/wazee/waangalizi wana mamlaka juu ya makanisa yao, sawa na jinsi ambavyo baba ana mamlaka juu ya familia yake.
Basi imempasa askofu [mchungaji/mzee] awe mtu asiyelaumika. … Mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) (1Timo. 3:2-5. Maneno mepesi kukazia).
Paulo akaendelea kusema hivi:
Wazee [wachungaji/waangalizi] watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha (1Timo. 5:17. Maneno mepesi kukazia).
Ni dhahiri kwamba wazee wanapaswa kutawala au kusimamia kanisa.
Wazee Kinyume Na Maandiko
Makanisa mengi yanaamini mpango wao wa utawala ni wa KiBiblia kwa sababu wana kundi la wazee wanaosimamia, lakini, tatizo ni kwamba wazo lao la wazee si sahihi. Wazee wao huchaguliwa kila mara na hubadilishana nafasi kutoka katika kusanyiko. Mara nyingi wanaitwa “Baraza la Wazee.” Lakini watu hao si wazee kulingana na tafsiri ya Biblia. Tukitazama sifa ambazo Paulo anataja kwa ajili ya mtu kuwa mzee, hilo linaonekana wazi kabisa. Paulo aliandika kwamba mzee hushikilia nafasi ya kudumu ya kufundisha na kuhubiri na kusimamia katika kanisa, na kwa maana hiyo analipwa (ona 1Timo. 3:4-5; 5:17-18; Tito 1:9). Katika watu wanaosemekana ni “Baraza la Wazee” kwenye makanisa mengi, ni wachache sana – kama wapo basi – ambao wanatimiza sifa hizo. Hawalipwi; hawahubiri wala kufundisha; si wafanya kazi wa kanisa; na wala hawajui jinsi ya kusimamia au kutawala kanisa.
Utawala wa kanisa ambao si wa kiMaandiko ndiyo sababu ya matatizo mengi sana kanisani kuliko kitu kingine chochote. Wakati watu wasiostahili wanaposimamia kanisa, shida ziko njiani. Mlango hufunguka kwa ajili ya vurugu, faraka na hata kuangamia kabisa kwa kanisa. Mpango wa utawala wa kanisa ambao si kulingana na Maandiko ni kama mkeka wa ukaribisho kwa Shetani.
Natambua kwamba nawaandikia wachungaji wa makanisa jengo na wa makanisa yanayokutanikia nyumbani. Baadhi ya wachungaji wa makanisa jengo wanaweza kuwa wanaongoza makanisa ambayo mfumo wa uongozi si wa kiMaandiko, ambapo wazee huchaguliwa kutoka katika kusanyiko. Mifumo hiyo haiwezi kubadilishwa bila ya kuleta vurugu.
Ushauri wangu kwa wachungaji kama hao ni huu: Fanya vizuri uwezavyo kwa msaada wa Mungu kubadilisha mfumo wa utawala wa kanisa, na uvumilie vurugu za muda zitakazotokea, maana vurugu za kudumu zinazokuja baadaye hazitaweza kuepukika kama hutafanya chochote sasa. Ukifanikiwa kuvumilia vurugu za muda, utajikuta umeepukana na vurugu zote za baadaye. Ukishindwa, anzisha kanisa jipya mahali na kufuata mpango wa Biblia.
Japo hilo linaumiza, mwisho wa siku utazaa matunda mengi zaidi kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Kama wale wanaotawala kanisa lako kwa sasa ni wafuasi wa kweli wa Kristo, unayo nafasi nzuri tu ya kufanikiwa kuwashawishi kubadilisha mfumo, kama utaweza kuwaonyesha kutoka Maandiko kinachopaswa, na jinsi ya kufanya hayo mabadiliko yanayohitajika sana.
Wazee Wengi Je?
Kuna wenye kuonyesha kwamba katika Maandiko wazee hutajwa katika wingi. Hoja hapo ni kwamba kuwa na mzee/mchungaji/mwangalizi mmoja anayesimamia kundi si kimaandiko. Huo si ushahidi wa kutosha kuamua kitu hicho. Kweli Biblia inataja kwamba, katika miji fulani fulani, waliokuwa wanasimamia kanisa walikuwa zaidi ya mzee mmoja, lakini haisemi kwamba hao wazee walikuwa wote wanalingana kimadaraka katika kusanyiko hilo. Kwa mfano: Wakati Paulo alipokusanya wazee kutoka Efeso (Matendo 20:17), ni dhahiri kwamba hao wazee walitoka kwenye mji ambao pengine kanisa lilikuwa na washirika maelfu kwa makumi elfu (ona Matendo 19:19). Basi, yawezekana kulikuwa na makundi mengi katika Efeso, na inawezekana kila mzee mmoja alisimamia kanisa moja.
Katika Maandiko, hakuna mahali popote ambapo Mungu aliita kamati ifanye kazi yoyote. Wakati alipotaka kutoa Waisraeli Misri, alimwita Musa – mtu mmoja – awe kiongozi. Wengine waliitwa kumsaidia Musa, lakini wote walikuwa chini yake kimadaraka, nao kama yeye walikuwa na majukumu binafsi juu ya kundi fulani la watu. Mtindo huo unapatikana katika Maandiko mara kwa mara. Wakati Mungu anapokuwa na kazi, anamwita mtu mmoja kuwajibika, kisha anamwita mwingine kumsaidia huyo.
Basi, haiwezekani kwamba Mungu anaweza kuita kamati ya wazee wenye mamlaka sawa ili kusimamia kila kanisa dogo linalokutania nyumbani, la watu ishirini. Hapo ni kama mwaliko kwa watu kuvurugana!
Lakini – hiyo haimaanishi kwamba kila kanisa la nyumbani lisimamiwe na mtu mmoja tu – mzee mmoja. Ila, maana yake ni kwamba, kama kuna mzee zaidi ya mmoja katika kanisa, yule ambaye ni kijana na asiyekomaa kiroho awe tayari kunyenyekea chini ya yule aliye mkubwa na aliyekomaa kiroho. Kulingana na Maandiko, makanisa ndiyo yanatakiwa kuwa maeneo ya kufundishia wachungaji vijana/wazee/waangalizi – si Shule za Biblia. Basi, inawezekana kabisa na inatakiwa kwamba wawepo wazee/wachungaji/waangalizi kadhaa katika kanisa la mahali, na wale ambao ni wadogo kiroho wafundishwe na wale ambao ni wakubwa kiroho.
Mambo hayo utayaona hata katika makanisa yanayodaiwa kusimamiwa na wazee “wanaolingana”. Yupo mmoja ambaye kila mara anapewa nafasi kubwa na wale wenzake. Au utakuta kuna mmoja ambaye ni kama mkuu, huku wengine wakiwa watazamaji tu. Vinginevyo kutakuwa na vurugu tu. Ni ukweli pia kwamba hata kamati huchagua mtu mmoja kuwa mwenyeketi. Wakati kundi la watu wanaolingana wanapochukua hatua ya kufanya kitu, wanatambua kwamba lazima kuwe na kiongozi mmoja. Ndivyo ilivyo pia kanisani.
Tena, Paulo analinganisha majukumu ya wazee na majukumu ya baba katika 1Timotheo 3:4, 5. Wazee lazima wasimamia nyumba zao, la sivyo hawafai kusimamia kanisa. Lakini tujiulize: Nyumba yenye baba wawili wenye mamlaka sawa itasimamiwaje? Bila shaka kutakuwa na matatizo.
Wazee/wachungaji/waangalizi wanapaswa kuunganika katika kusanyiko la mahali ili kuwe na uwajibikaji mmoja kwa mwingine miongoni mwao, ili kama kuna tatizo, waweze kusaidiana. Paulo aliandika kuhusu “wazee” (ktk 1Timo. 4:14). Pengine maana yake ni mkutano au mkusanyiko wa presbuteros (wazee) pamoja na watu wengine wenye karama za huduma. Kama kuna mtume mwanzilishi, yeye pia anaweza kutoa msaada ikiwa kuna matatizo katika kusanyiko, yanayotokana na mzee aliyekosea. Wachungaji wenye makanisa jengo wanapopotoka, matokeo yake huwa ni matatizo makubwa kwa sababu ya mfumo wa kanisa. Kuna jengo na taratibu za kufuata. Lakini, makanisa yanayokutanika nyumbani yanaweza kuvunjwa mara moja wakati mchungaji anayehusika anapopotoka. Washirika watajiunga na kundi lingine.
Mamlaka Ya Kutumika
Kwa kuwa Mungu anampa mchungaji mamlaka ya kiroho na kusimamia kanisani mwake, hili halimpi haki ya kutawala kwa nguvu kundi lake. Yeye si Bwana wao – Bwana wao ni Yesu. Wao si kundi lake – ni kundi la Mungu.
Lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka (1Petro 5:2-4. Maneno mepesi kukazia).
Kila mchungaji atatoa hesabu ya huduma yake siku moja, mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo.
Tena, kwa habari ya fedha, mchungaji/mzee/mwangalizi asifanye kitu peke yake. Kama kuna fedha zinakusanywa kila mara au mara kwa mara kwa sababu yoyote ile, wengine katika kusanyiko wawajibike ili kusiwe na kutoaminiana kuhusu matumizi ya fedha (ona 2Wakor. 8:18-23). Hao wengine wawe kundi lililochaguliwa au kuteuliwa.
Kulipa Wazee
Maandiko yanaonyesha wazi kwamba wazee/waangalizi/wachungaji wanapaswa kulipwa, maana ni watenda kazi wa kudumu wa kanisa. Kwa habari hii, Paulo aliandika kama ifuatavyo:
Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hawa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha. Kwa maana andiko lasema, ‘Usimfunge kinywa ng’ombe apurapo nafaka.’ Na tena, ‘Mtenda kazi astahili ujira wake.’ (1Timo. 5:17, 18).
Mada iko wazi kabisa – na Paulo anatumia neno ujira. Maneno yake yasiyokuwa wazi sana kuhusu wazee watawalao vema wahesabiwe kustahili heshima maradufu yanaeleweka kirahisi wakati mantiki inapotazamwa. Katika mistari kabla ya hii, Paulo anaandika waziwazi kuhusu jukumu la kanisa kuwasaidia kifedha wajane ambao wasingepata msaada kwa njia nyingine, na anaanza kwa maneno yale yale: “Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli” (ona 1Timo. 5:3-36). Basi, katika mantiki hii, “kuheshimu” maana yake ni kuwasaidia kifedha. Wazee wanaotawala vema wahesabiwe kustahili heshima mara mbili, yaani, wapokee mara mbili ya kiasi ambacho wajane wanapewa, na hata zaidi kama wana watoto wanaowategemea.
Makanisa jengo katika dunia nzima huwategemeza kifedha wachungaji wao (hata katika mataifa maskini), lakini inaonekana makanisa mengi yanayokutania nyumbani duniani kote – hasa nchi za Magharibi – hayafanyi hivyo. Hii ni kwa sababu ya ukweli kwamba makusudi hasa ya watu wengi katika nchi za Magharibi ya kujiunga na makanisa ya nyumbani ni uasi moyoni, nao wanatafuta na wamepata Ukristo usio na masharti mengi. Wanasema walijiunga na kanisa la nyumbani kwa sababu walitaka kuepukana na kifungo cha kanisa jengo, lakini ukweli ni kwamba walitaka kuepukana na aina yoyote ya kujitoa kikamilifu kwa Kristo. Wamepata makanisa yasiyotaka watu wajitolee kifedha, makansia yenye kwenda kinyumke kabisa na kile ambacho Kristo anatazamia kwa wanafunzi Wake. Hayo, mungu wao ni fedha, na wanathibitisha hilo kwa kujilundia hazina zao duniani badala ya mbinguni. Hao si wanafunzi wa kweli wa Kristo (ona Mathayo 6:19-24; Luka 14:33). Kama Ukristo wa mtu hauathiri anachofanya na fedha zake, huyo si Mkristo kabisa.
Makanisa yanayokutania nyumbani yenye kudai kwamba ni ya KiBiblia yanapaswa kuwatunza wachungaji wao kifedha, na kuwasaidia maskini na kusaidia kazi ya utume. Kwa kutoa na katika mambo yote yakifedha, wanapaswa kuzidi sana makanisa jengo, maana wao hawana majengo ya kulipia wala watumishi wengi wa kulipa mishahara. Wanahitajika watu kumi tu ambao watatoa zaka ili kumtunza mchungaji mmoja. Watu kumi wanaotoa asilimia ishirini ya mapato yao wanaweza kumtegemeza vizuri sana mchungaji mmoja na mishenari mmoja atakayeishi kwenye kiwango kile cha mchungaji wao.
Wachungaji Hufanya Nini?
Fikiri kwamba unamwuliza mshirika wa kawaida kanisani swali hili: “Je, ni kazi ya nani kufanya yafuatayo:- kuwashuhudia watu ambao hawajaokoka? Kuishi maisha matakatifu? Kuomba? Kuonya, kushauri na kusaidia waamini wengine? Kutembelea wagonjwa? Kuweka mikono juu ya wagonjwa kwa ajili ya uponyaji? Kubeba mizigo yaw engine? Kutumia karama zake kwa ajili ya kusanyiko? Kujikana, akijitoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu? Kufanya wanafunzi na kuwabatiza, na kuwafundisha kutii amri za Kristo?”
Washirika wengi wa kanisa, bila ya kusita, wangejibu kwa kusema, “Hayo yote ni majukumu ya mchungaji.” Lakini, ni sawa?
Kulingana na Maandiko, kila aaminiye anapaswa kuwashuhudia watu ambao hawajaokoka.
Mwe tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu (1Petro 3:15).
Kila aaminiye anawajibika kuishi matisha matakatifu.
Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, ‘Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu’ (1Petro 1:15, 16).
Kila mwamini anatakiwa kuomba.
Furahini sikuzote. Ombeni bila kukoma (1Wathes. 5:16, 17).
Kila aaminiye anatazamiwa kuonya, kutia moyo na kuwasaidia waamini wengine.
Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote (1Wathes. 5:14. Maneno mepesi kukazia).
Kila aaminiye anatakiwa kutembelea wagonjwa.
Nalikuwa uchi, mkanivika. Nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama. Nalikuwa kifungoni, mkanijia (Mathayo 25:36).
Majukumu Zaidi
Lakini, si hayo tu. Kila aaminiye anapaswa kuweka mikono juu ya wagonjwa na kuwaponya pia.
Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio. Kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona (Marko 16:17, 18. Maneno mepesi kukazia).
Kila aaminiye anapaswa kubeba mizigo ya waamini wenzake.
Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo (Wagalatia 6:2).
Kila aaminiye anatazamiwa kutumia karama zake kwa ajili ya wengine.
Basi, kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha katika kufundisha kwake; mwenye kuonya katika kuonya kwake; mwenye kukirimu kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii; mwenye kurehemu kwa furaha (Warumi 12:6-8).
Kila mwamini anapaswa kujikana mwenyewe, na kujitoa kwa ajili ya Injili.
Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, ‘Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha’ (Marko 8:34, 35. Maneno mepesi kukazia).
Tena, kila mwamini anatazamiwa kufanya watu kuwa wanafunzi, na kuwabatiza, na kuwafundisha kutii amri zote za Kristo.
Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni (Mathayo 5:19. Maneno mepesi kukazia).
Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu (Waebrania 5:12. Maneno mepesi kukazia).
Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi. Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari (Mathayo 28:19, 20. Maneno mepesi kukazia).[2]
Majukumu hayo yote yametolewa kwa kila aaminiye, lakini washirika wengi wa kanisa hufikiri kwamba yametolewa kwa wachungaji tu! Pengine sababu ni kwamba wachungaji wengi pia hufikiri kwamba hayo ni majukumu yao peke yao.
Basi, Wachungaji Wanapaswa Kufanya Nini?
Kama majukumu hayo yote yametolewa kwa kila aaminiye, wachungaji basi wanatakiwa kufanya nini? Kirahisi tu ni kwamba, wao wameitwa kuwawezesha hao waaminio watakatifu kufanya mambo hayo yote (ona Waefeso 4:11, 12). Wameitwa kuwafundisha hao waaminio watakatifu kutii amri zote za Kristo (ona Mathayo 28:19, 20) kwa kuonyesha mfano pamoja na kufundisha (ona 1Timo. 3:2; 4:12, 13; 5:17; 2Timo. 2:2; 3:16 – 4:4; 1Petro 5:1-4).
Maandiko hayawezi kuwa wazi kuliko hivyo. Nafasi ya KiBiblia ya mchungaji sio kukusanya watu wengi kiasi anachoweza Jumapili asubuhi kwenye ibada kanisani. Ni “kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo” (Wakolosai 1:28). KiBiblia, wachungaji hawatekenyi masikio ya watu (2Timo. 4:3). Wanafundisha, wanaonya, wanakemea, wanakaripia, na kurekebisha, na yote hufanywa kwa msingi wa Neno la Mungu (ona 2Timo. 3:16 – 4:4).
Paulo aliorodhesha baadhi ya sifa za mtu anayetaka kusimama katika nafasi ya mchungaji, katika barua yake ya kwanza kwa Timotheo. Sifa kumi na nne kati kumi na tano zinahusu tabia yake, kuonyesha kwamba mfano wa maisha yake ndicho kitu cha muhimu zaidi sana.
Ni neno la kuainiwa [kwamba] mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kusimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) Wala asiwe mtu aliyeongoka karibuni, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi (1Timo. 3:1-7).
Ukifananisha sifa hizi na zile ambazo mara nyingi hutolewa na makanisa yanapotafuta mchungaji mpya utagundua tatizo la msingi katika makanisa mengi. Wao hutafuta meneja wa kusimamia wafanyakazi/mtu wa kustarehesha watu/mtoa hotuba fupi/msimamizi/mwanasaikolojia/mkurugenzi wa shughuli na mipango/bingwa wa kuchangisha fedha/rafiki wa kila mtu/farasi au punda wa kazi. Wanataka mtu “wa kuendesha huduma ya kanisa.” Lakini, mwangalizi KiBiblia, zaidi ya yote lazima we mtu mwenye tabia nzuri na aliyejitolea kwa Kristo, awe mtumishi wa kweli kwa sababu lengo lake ni kujizaa mwenyewe. Lazima aweze kuwaambia washirika wake, “Niigeni mimi, kama na mimi ninavyomwiga Kristo” (1Wakor. 11:1).
Kwa maelezo zaidi kuhusu nafasi ya mchungaji, soma pia maandiko yafuatayo: Matendo 20:28-31; 1Timo. 5:17-20; na Tito 1:5-9.
Nafasi Ya Shemasi
Mwisho, hebu tutazame kidogo habari za shemasi. Nafasi ya sehmasi ni nafasi nyingine katika kanisa la mahali ambayo si miongoni mwa zile karama tano za huduma. Mashemasi si kama wazee – wao hawana mamlaka ya kiutawala katika kanisa. Neno la Kiyunani diakonos ambalo limetafsiriwa shemasi maana yake ni “mtumishi” au “atoaye huduma”.
Wale watu saba waliochaguliwa kwa ajili ya kazi ya kuwalisha wajane wa kanisa la Yerusalemu kila siku ndiyo huhesabiwa kuwa mashemasi wa kwanza (ona Matendo 6:1-6). Walichaguliwa na kusanyiko na kupewa kazi na mitume. Wawili wao – Filipo na Stefano – walipandishwa cheo na Mungu, wakawa wainjilisti wenye nguvu sana.
Pia, mashemasi wanatajwa katika 1Timo. 3:8-13 na Wafilipi 1:1. Tena, inaonekana nafasi hii inaweza kuchukuliwa na mwanamume au mwanamke (ona 1Timo. 3:11).
[1] Hiyo ni njia nyingine ya kusema hivi: “Kwa ajili ya kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo.”
[2] Kama wanafunzi wa Yesu walitazamiwa kuwafundisha wanafunzi wao kutii kila kitu Yeye alichowaamuru, basi bila shaka wangewafundisha wanafunzi wao jinsi ya kufanya wengine kuwa wanafunzi pia, na kubatiza na kuwafundisha kuyashika yote ambayo Yesu aliamuru. Hivyo, kufanya wanafunzi, kubatiza na kufundisha wanafunzi ingekuwa amri inayoendelea, na inayofanya kazi kwa kila mwanafunzi aliyefuata.