Katika nyaraka za Agano Jipya, tunakutana na maneno “ndani ya Kristo”,
“pamoja na Kristo,” “kwa njia ya Kristo,” na “ndani Yake.” Mara nyingi, maneno hayo yanadhihirisha manufaa fulani ambayo sisi kama waamini tunayo kwa sababu ya mambo Yesu aliyotutendea. Tunapojiona kama Mungu anavyotuona – “ndani ya Kristo” – itatusaidia kuishi kama Mungu anavyotaka. Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi atataka kuwafundisha wanafunzi wake nafasi yao katika Kristo, ili kuwasaidia wakue na kukomaa kiroho.
Kwanza: Nini maana ya kuwa “ndani ya Kristo”?
Tunapozaliwa mara ya pili, tunaingizwa katika mwili wa Kristo na kuwa wamoja Naye kiroho. Hebu tutazame mistari kadha katika nyaraka za Agano Jipya yenye kuthibitisha hicho.
Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo (Warumi 12:5. Maneno mepesi kukazia).
Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye (1Wakor. 6:17. Maneno mepesi kukazia).
Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungokila mmoja peke yake (1Wakor. 12:27. Maneno mepesi kukazia).
Sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo tunapaswa kujiona kwamba tumeunganishwa Naye, ni viungo vya mwili Wake na ni wamoja na Yeye katika roho. Yeye yu ndani yetu, nasi tu ndani Yake.
Angalia mstari huu unaotuambia baadhi ya manufaa tuliyo nayo kwa sababu ya kuwa ndani ya Kristo.
Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi (1Wakor. 1:30. Maneno mepesi kukazia).
Katika Kristo, tumefanywa kuwa wenye haki (yaani, tumehesabiwa “hatua hatia” na sasa tunatenda yaliyo sawa), tumetakaswa (yaani, tumetengwa kwa ajili ya Mungu kututumia katika kazi takatifu), na tumekombolewa (yaani, tumenunuliwa kutoka utumwani). Si kwamba tunangojea kufanywa wenye haki, au kutakaswa au kukombolewa wakati fulani katika siku za baadaye. Ni kwamba sasa hivi sisi tunazo baraka hizo zote, kwa kuwa tuko ndani ya Kristo.
Katika Kristo, dhambi zetu za zamani zimesamehewa zote.
Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani msamaha wa dhambi (Wakolosai 1:13, 14. Maneno mepesi kukazia).
Ona kwamba mstari huu unatuambia pia kwamba hatuko tena katika ufalme wa Shetani – utawala wa giza – bali sasa tuko katika ufalme wa nuru, ufalme wa Yesu.
Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya (2Wakor. 5:17. Maneno mepesi kukazia).
Msifu Mungu kwamba, kama wewe ni mfuasi wa Kristo, ni “kiumbe kipya” sawa na buu aliyebadilika na kuwa kipepeo! Roho yako imepewa asili mpya. Hapo kwanza ulikuwa na asili ya Shetani ya ubinafsi ndani ya roho yako, lakini sasa maisha yako yote ya kale “yamepita”.
Baraka Zaidi Katika Kristo
Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu (Wagalatia 3:26. Maneno mepesi kukazia).
Ni raha sana kujua kwamba sisi ni watoto wa Mungu mwenyewe, tuliozaliwa kwa Roho Wake! Tunapomwendea katika maombi, tunamwendea – si kama Mungu wetu tu – bali pia kama Baba yetu!
Maana tu kazi Yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo (Waefeso 2:10. Maneno mepesi kukazia).
Mungu hakutuumba tu. Ametuumba upya katika Kristo. Tena, Mungu ametupangia huduma ya kutimiza kila mmoja wetu, “matendo mema … tokea awali.” Kila mmoja wetu ana karima yake binafsi, iliyoandaliwa na Mungu Mwenyewe!
Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika yeye (2Wakor. 5:21. Maneno mepesi kukazia).
Haki tuliyo nayo kwa sababu tuko ndani ya Kristo ni haki ya Mungu Mwenyewe. Hii ni kwa sababu Mungu amekaa ndani yetu na kutubadilisha kwa Roho Mtakatifu. Ukweli ni kwamba matendo yetu mema ni yale ya Mungu, kupitia kwetu.
Lakini katika mambo hayo yote tunashinda na zaidi ya kushinda kwa Yeye aliyetupenda (Warumi 8:37. Maneno mepesi kukazia).
Hayo “mambo yote” ambayo Paulo anasema, ni yapi? Mistari katika Warumi inayotangulia mstari huu inadhihirisha kwamba ni yale majaribu na kuteseka ambako waamini hupata. Hata katika kufa kwa ajili ya imani, bado sisi ni washindi, ingawa dunia inaweza kuhesabu kwamba tumeshindwa. Tunashinda na zaidi ya kushinda kwa Kristo kwa sababu, tunapokufa, tunakwenda mbinguni!
Nayaweza mambo yote katika Yeye anitiaye nguvu (Wafilipi 4:13. Maneno mepesi kukazia).
Kwa njia ya Kristo, hakuna kisichowezekana kwetu kwa sababu Mungu anatuwezesha na kututia nguvu. Tunaweza kufanikisha kazi yoyote atakayotupa.
Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu (Wafilipi 4:19. Maneno mepesi kukazia).
Tutazamie kwamba Mungu atakutana na mahitaji yetu halisi, kama tutatafuta kwanza ufalme Wake. Bwana ndiye mchungaji wetu, naye huwatunza kondoo Wake!
Kukubaliana Na Anachosema Mungu
Kwa bahati mbaya, baadhi yetu hatuamini kile ambacho Neno la Mungu linasema juu yetu. Hayo huonekana kwa maneno kinyume tunayotamka, yenye kupingana na kinachosemwa na Biblia. Badala ya kusema, “Nayaweza mambo yote katika Kristo anitiaye nguvu,” sisi husema, “Sidhani kama nitaweza.”
Maneno kama hayo ndiyo Biblia inayaita “taarifa mbaya” kwa sababu hayakubaliani na kile anachosema Mungu (ona Hesabu 13:32). Lakini, kama mioyo yetu imejaa Neno la Mungu, tutajaa imani, na kuamini na kusema yale tu yanayokubaliana na Maandiko.
Matamko Machache Ya Biblia
Tunapaswa kuamini na kusema kwamba sisi tuko kama Mungu anavyosema.
Tunapaswa kuamini na kusema kwamba tunaweza kufanya yale Mungu anayosema tunaweza kufanya.
Tunapaswa kuamini na kusema kwamba Mungu yuko kama anavyosema.
Tunapaswa kuamini na kusema kwamba Mungu atafanya alichosema atafanya.
Yafuatayo ni matamko ya Maandiko ambayo waamini wote wanaweza kuyakiri kwa ujasiri kabisa. Si yote yanayohusu “kuwa ndani ya Kristo”, lakini yote ni kweli kulingana na Maandiko.
Nimekombolewa, nimetakaswa na kuhesabiwa haki katika Kristo (ona 1Wakor. 1:30).
Nimehamishwa kutoka ufalme wa giza na kuingizwa katika ufalme wa Mwan wa Mungu, yaani ufalme wa nuru (ona Wakolosai 1:13).
Dhambi zangu zote zimesamehewa katika Kristo (ona Waefeso 1:7).
Mimi ni kiumbe kipya ndani ya Kristo – maisha yangu ya kale yamepita (2Wakor. 5:17).
Mungu ameniandalia kabla matendo mema, ili nienende ndani yake (ona Waefeso 2:10).
Nimefanyika haki ya Mungu katika Kristo (ona 2Wakor. 5:21).
Mimi ni mshindi katika mambo yote kwa njia ya Kristo aliyenipenda (ona Warumi 8:37).
Naweza kufanya mambo yote kwa njia ya Kristo anitiaye nguvu (ona Wafilipi 4:13).
Mungu wangu hunipa mahitaji yangu yote kulingana na utajiri wake katika utukufu, katika Kristo (ona Wafilipi 4:19).
Nimeitwa kuwa mtakatifu (ona 1Wakor. 1:2).
Mimi ni mtoto wa Mungu (ona Yohana 1:12; 1Yohana 3:1, 2).
Mwili wangu ni hekalu la Roho Mtakatifu (ona 1Wakor. 6:19).
Si mimi ninayeishi tena, bali Kristo ndani yangu (ona Wagalatia 2:20).
Nimekombolewa kutoka mamlaka ya Shetani (ona Matendo 26:18).
Upendo wa Mungu umemiminwa moyoni mwangu na Roho Mtakatifu (ona Warumi 5:5).
Aliye ndani yangu ni mkuu kuliko (Shetani) aliyeko duniani (ona 1Yohana 4:4).
Nimebarikiwa kwa baraka zote za kiroho na kuketishwa mbinguni katika Kristo (ona Waefeso 1:3).
Nimeketi pamoja na Kristo mbinguni, juu sana kuliko majeshi yote ya kiroho ya Shetani (ona Waefeso 2:4-6).
Kwa kuwa nampenda Mungu na nimeitwa kulingana na kusudi Lake, anafanya mambo yote kuwa mema kwa ajili yangu (ona Warumi 8:28).
Kama Mungu yuko upande wangu, nani anayeweza kuwa kinyume changu? (ona Warumi 8:31).
Hakuna kinachoweza kunitenga na upendo wa Kristo (ona Warumi 8:35-39).
Yote yanawezekana kwangu kwa sababu mimi ni mwamini (ona Marko 9:23).
Mimi ni kuhani wa Mungu (ona Ufunuo 1:6).
Kwa kuwa ni mtoto Wake, Mungu ananiongoza kwa Roho Wake (ona Warumi 8:14).
Ninapoendelea kumfuata Bwana, njia ya maishayangu inazidi kung’aa (ona Mithali 4:18).
Mungu amenipa karama za pekee kutumia kwa ajili ya huduma Yake (ona 1Petro 4:10, 11).
Naweza kutoa pepo na kuweka mikono yangu juu ya wagonjwa, wapone (ona Marko 16:17, 18).
Kila mara, Mungu huniongoza kushinda katika Kristo (ona 2Wakor. 2:14).
Mimi ni balozi wa Kristo (ona 2Wakor. 5:20).
Nina uzima wa milele (ona Yohana 3:16).
Kila niombacho, nikiamini, ninakipokea (ona Mathayo 21:22).
Kwa kupigwa kwa Yesu nimeponywa (ona 1Petro 2:24).
Mimi ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu (ona Mathayo 5:13, 14).
Mimi ni mrithi wa Mungu, na mrithi pamoja na Yesu Kristo (ona Warumi 8:17).
Mimi ni mteule, ni ukuhani wa kifalme, ni taifa takatifu, ni milki ya Mungu (ona 1Petro 2:9).
Mimi ni kiungo cha mwili wa kristo (ona 1Wakor. 12:27).
Bwana ni mchungaji wangu, sitahitaji kitu (ona Zaburi 23:1).
Bwana ndiye mlinzi wa maisha yangu – nimwogope nani? (ona Zaburi 27:1).
Mungu atanishibisha maisha marefu (ona Zaburi 91:16).
Kristo alichukua magonjwa yangu na maumivu yangu (ona Isaya 53:4, 5).
Bwana ndiye anisaidiaye – sitaogopa (ona Waebrania 13:6).
Namtwika Bwana fadhaa zangu zote, maana Yeye ananijali sana (ona 1Petro 5:7).
Nampinga Shetani, naye ananikimbia (ona Yakobo 4:7).
Ninapata maisha yangu kwa kuyapoteza kwa ajili ya Yesu (ona Mathayo 16:25).
Mimi ni mtumwa wa Bwana (ona 1Wakor. 7:22).
Kwangu, kuishi ni Kristo na kufa ni faida (ona Wafilipi 1:21).
Uraia wangu ni mbinguni (ona Wafilipi 3:20).
Mungu ataimaliza kazi njema aliyoanza ndani yangu (ona Wafilipi 1:6).
Mungu yuko ndani yangu akitenda kazi (ona Wafilipi 2:13).
Nimekombolewa kutokana na laana ya Torati (ona Wagalatia 3:13).
Hayo ni machache tu kati ya matamko mengi sahihi tunayoweza kufanya, kutoka katika Neno la Mungu. Itakuwa jambo jema kujenga tabia ya kutamka hayo mara kwa mara mpaka kweli zake zipate kina na mizizi ndani ya mioyo yetu. Nasi tunapaswa kuchunga kila neno litokalo katika midomo yetu ili tuhakikishe kwamba hatusimami kinyume na maneno ambayo Mungu amesema.