Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi. Tena, mmeyasahau yale maonyo yasemayo nanyi kama kusema na wana, ‘Mwanangu! Usiyadharau marudia ya Bwana, wala usizimie moyo ukikemewa naye. Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, naye humpiga kila mwana amkubaliye. ‘ Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili, Mungu awatendea kama wana. Maana, ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo, tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi. Basi, si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika, hao kwa siku cahche waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani. Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza, mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kipone (Waebrania 12:3-13).
Kulingana na mwandishi aliyevuviwa wa Kitabu cha Webrania, Baba yetu wa mbinguni huwaadhibu watoto Wake wote. Tusipoadhibiwa Naye, maana yake ni kwamba sisi si watoto Wake. Basi tunahitaji kuwa makini na kujua kuhusu adhabu Zake. Kuna Wakristo wengine ambao mtazamo wao wa peke ni baraka za Mungu na wema Wake tu, wanaotafsiri mazingira yote ambayo ni kinyume kuwa ni mashambulizi toka kwa Shetani, yasiyokuwa na mpango wowote wa kiMungu. Hili linaweza kuwa kosa kubwa sana, kama Mungu anajaribu kuwafikisha kwenye toba kwa kutumia adhabu Zake.
Wazazi wazuri wa kidunia hutoa adhabu kwa watoto wao kwa matumaini kwamba hao watajifunza, watakomaa na kuwa tayari kuwa watu wazima wenye kuwajibika maishani. Mungu pia hutuadhibu ili tukue kiroho, tufae katika huduma Yake zaidi, na tuwe tayari kusimama mbele ya kiti Chake cha hukumu. Anatuadhibu kwa sababu anatupenda, na kwa sababu anatamani tushiriki utakatifu Wake. Baba yetu wa mbinguni mwenye upendo anataka sana tukue kiroho. Maandiko yanasema hivi: “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya KristoYesu” (Wafilipi 1:6).
Hakuna mtoto anayefurahia viboko vya wazazi wake. Na sisi, tunapoadhibiwa na Mungu, jambo hilo “si la furaha bali la huzuni” kama tulivyosoma. Ila mwishowe, mambo yanakuwa mazuri kwa sababu nidhamu (au adhabu hiyo) “husababisha tunda la amani la haki”.
Je, Mungu Hutuadhibu Lini, Kwa Njia Gani?
Kama baba mzuri, Mungu huwaadhibu watoto Wake wakati wanapoacha kutii. Wakati wowote tunapoacha kumtii, tuko hatarini kuadhibiwa. Ila, Bwana ni mwenye rehema sana, naye mara nyingi hutupa muda mrefu wa kutubu. Adhabu yake mara nyingi huja baada ya sisi kurudia kutokutii, na Yeye kutuonya mara nyingi.
Je, Mungu anatuadhibu namna gani? Kama tulivyojifunza katika sura mojawapo huko nyuma, adhabu ya Mungu inaweza kuja kama udhaifu fulani, ugonjwa au hata kufa kabla ya wakati.
Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa. Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia (1Wakor. 11:30-32).
Hatupaswi kuamua kwamba kila ugonjwa ni matokao ya adhabu ya Mungu (hapa kumbuka swala la Ayubu). Lakini, ugonjwa ukija, ni vizuri kufanya ukaguzi kiroho ili kuona kama labda tumefungua mlango wa adhabu ya Mungu kwa kutokutii.
Twaweza kuepukana na hukumu ya Mungu kama tutajihukumu wenyewe – yaani, tukiri dhambi yetu na kuitubu. Ni dhahiri kwamba tutajikuta tunaponywa mara tu baada ya kutubu, ikiwa ugonjwa wetu ni matokeo ya adhabu ya Mungu.
Paulo anasema kwamba tunapohukumiwa na Mungu, tunaepuka kuhukumiwa pamoja na dunia. Je, alimaanisha nini? Bila shaka alimaanisha kwamba adhabu ya Mungu hutuongoza sisi kutubu ili hatimaye tusitupwe jehanamu pamoja na watu wa dunia. Hili ni gumu kukubalika na wale wanaofikiri kwamba utakatifu ni kitu cha hiari kwa wale wanaokwenda mbinguni. Lakini, kwa wale waliosoma Mahubiri ya Yesu Mlimani, wanajua kwamba wale tu wanaomtii Mungu ndiyo watakaoingia katika ufalme Wake (ona Mathayo 7:21). Basi, tukidumu katika dhambi na tusitubu, tuko hatarini kukosa uzima wa milele. Bwana asifiwe kwa adhabu Yake, inayotuongoza kutubu, na kutuokoa na jehanamu!
Shetani Kama Chombo Kwa Ajili Ya Hukumu Ya Mungu
Ni dhahiri kutokana na maandiko mengi kwamba Mungu anaweza kumtumia Shetani kwa ajili ya kutimiza adhabu Zake. Kwa mfano: Katika mfano wa mtumwa asiyesamehe upatikanao katika Mathayo 18, Yesu anasema kwamba bwana wa mtumwa yule “akaghadhabika sana” baada ya kufahamu kwamba mtumwa wake aliyemsamehe hakumsamehe mwenzake. Basi, akamtoa kwa “watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote” (Mathayo 18:34). Yesu alimalizia mfano huu kwa maneno haya mazito:
Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake (Mathayo 18:35).
Sasa – hao “watesaji” ni akina nani? Inaonekana ni Shetani na mapepo yake. Mungu anaweza kumtoa mmoja wa watoto Wake wasiokuwa watiifu kwa Shetani, ili kumfikisha mahali pa kutubu. Magumu na majanga yana njia ya kuwafikisha watu kutubu – kama alivyojifunza mwana mpotevu (ona Luka 15:14-19).
Katika Agano la Kale tunapata mifano ya Mungu akimtumia Shetani au pepo wabaya ili kutimiza adhabu Yake au hukumu katika maisha ya watu waliostahili hayo. Mfano mmoja unapatikana katika Waamuzi sura ya tisa, tunaposoma kwamba, “Kisha Mungu akapeleka roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu” (Waamuzi 9:23) ili kuleta hukumu juu yao kwa sababu ya matendo yao maovu juu ya wana wa Gidioni.
Biblia pia inasema, “roho mbaya kutoka kwa Bwana” ilimsumbua mfalme Sauli ili kumfikisha kwenye toba (1Sam. 16:14). Ila, Sauli hakutubu, na mwishoni alikufa vitani kwa sababu ya uasi wake.
Katika mifano hiyo miwili ya Agano la Kale, Manadiko yanasema hizo roho mbaya (au pepo) “zilitumwa na Mungu.” Hii haimaanishi kwamba Mungu ana pepo mbinguni wanaosubiri kumtumikia. Pengine ni kwamba Mungu anaruhusu mapepo wa Shetani kufanya kazi yao mbaya kwa watu, kwa mipaka, kwa matumaini kwamba wenye dhambi watatubu kwa sababu ya mateso yao.
Njia Zingine Za Adhabu Ya Mungu
Katika Agano la Kale pia tunakuta kwamba Mungu aliwaadhibu watu Wake mara kwa mara kwa kuruhusu matatizo kama njaa au majeshi ya kigeni kutawala. Hatimaye wangetubu, Naye angewakomboa na adui zao. Walipokataa kutubu baada ya miaka mingi ya mateso na maonyo, Mungu alikuwa anaruhusu utawala wa kigeni kuwashinda kabisa na kuwahamisha kutoka nchi yao kama mateka.
Katika agano jipya, inawezekana kabisa Mungu kuwaadhibu watoto Wake wasiotii kwa kuruhusu matatizo kuingia maishani mwao. Au anaweza kuruhusu maadui zao kuwatesa. Kwa mfano: Maandiko tuliyoanza nayo sura hii kuhusu adhabu ya Mungu (Waebrania 12:3-13), yanapatikana katika mantiki ya waamini wa Kiebrania waliokuwa wanateswa kwa ajili ya imani yao. Ila, si mateso yote yanayoruhusiwa kwa sababu ya kutokutii. Kila jambo lipimwe peke yake.
Kuitikia Vizuri Adhabu Ya Mungu
Kulingana na ushauri uliotajwa mwanzoni mwa sura hii, tunaweza kuitikia vibaya adhabu ya Mungu kwa namna mojawapo kati ya hizi mbili. Tunaweza “kudharau marudia ya Bwana” au tunaweza “kuzimia moyo tukikemewa naye” (Waebrania 12:5). Kama tuta”dharau” marudia ya Bwana, maana yake ni kwamba hatuitambua adhabu yake, au ni kwamba tunapuuzia maonyo yake. Kuzimia moyo kutokana na adhabu ya Mungu ni kukata tamaa au kuacha kumpendeza kwa sababu tunaona adhabu Yake ni kali sana. Itikio lolote katika hayo ni kosa. Tunapaswa kutambua kwamba Mungu anatupenda, naye hutuadhibu kwa faida yetu. Tukitambua mkono Wake wa upendo katika adhabu, tunapaswa kutubu na kupokea msamaha Wake.
Baada ya kutubu, tutazamie nafuu kutoka kwa adhabu ya Mungu. Lakini, tusitazamie nafuu kutokana na matokeo mabaya na yasiyoepukika ya dhambi yetu, ingawa tunaweza kumwomba Bwana rehema na msaada Wake. Mungu huitikia moyo mnyenyekevu na uliopondeka (ona Isaya 66:2). Biblia inaahidi hivi, “Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo, katika radhi yake mna uhai. Huenda kilio huja kukaa usiku, lakini asubuhi huwa furaha” (Zaburi 30:5).
Baada ya hukumu Yake kuwashukia Israeli, Mungu aliahidi hivi:
Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya. Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu (Isaya 54:7, 8).
Mungu ni mwema, na mwenye rehema!
Kwa kujifunza zaidi kuhusu adhabu ya Mungu, ona maandiko yafuatayo: 2Nyakati 6:24-31, 36-39; 7:13, 14; Zaburi 73:14; 94:12, 13; 106:40-46; 118:18; 119:67, 71; Yeremia 2:29, 30; 5:23-25; 14:12; 30:11; Hagai 1:2-13; 2:17; Matendo 5:1-11; Ufunuo 3:19.